TIMU ya KMC hali yake imeendelea kuwa mabaya ikipoteza mchezo wa Ligi Kuu Bara ikiwa nyumbani dhidi ya JKT Tanzania kwa bao 1-0.
Matokeo hayo yanaifanya KMC kuendelea kujichimbia mkiani ikibaki na pointi tatu, ikipoteza mchezo wa sita mfululizo katika msimu huu.
Licha ya kuonyesha mchezo mzuri KMC imeendelea kuonyesha udhaifu kwenye safi yake ya ushambuliaji ikishindwa kutumia nafasi ilizotengeneza kufunga mabao ambayo yangeweza kuinasua.
Bao la kipindi cha pili lililotokana na krosi ya Anuary Kilemile katika dakika ya 61 kisha ikambabatiza beki wa KMC, Ibrahim Abbas ‘Nindi’ limetosha kuamua mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa KMC Complex.
JKT ingeweza kuongeza bao katika ushindi wake, lakini ikakosa utulivu kutumia nafasi zilizotengenezwa na mshambuliaji Paul Peter na kiungo Hassan Dilunga.
Ushindi huo unaifanya JKT kupaa kutoka nafasi ya saba mpaka ya pili ikifikisha pointi 10 sawa na vinara Yanga, ikicheza michezo saba, ikiishusha Simba kwa nafasi moja.
