Lishe bora shuleni yapewa kipaumbele Sumbawanga

Rukwa. Katika mwendelezo wa utekelezaji wa afua za lishe katika Wiki ya Lishe Kitaifa, Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imeendelea kuimarisha huduma za lishe shuleni kwa kugawa unga wenye virutubisho kwa shule za sekondari.

Jumla ya kilo 2,850 za unga zimetolewa kwa shule zote za sekondari za Manispaa, ambapo kila shule imepokea mifuko sita yenye uzito wa kilo 25 kila mmoja.

Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata mlo bora na wenye virutubisho muhimu kwa afya na maendeleo yao.

Halmashauri imeeleza kuwa utoaji wa unga huu ni sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha lishe shuleni, ukizingatia kuwa lishe bora ni msingi wa ukuaji wa mwili na ubongo wa mtoto.

Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa wanafunzi wanaopata chakula chenye mlo kamili hupata umakini zaidi darasani, hupunguza utoro, na huongeza ufaulu kwa ujumla.

Wa pili kushoto ni kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga Musa Musoma wakati akikabidhi unga wenye virutubisho katika shule ya sekondari Sumbawanga  Picha na Neema Mtuka

Pia, lishe duni imekuwa moja ya changamoto zinazoathiri maendeleo ya kitaaluma na kiafya kwa watoto, hivyo juhudi kama hizi zinatoa mchango mkubwa katika kuhakikisha mazingira ya ujifunzaji yanakuwa rafiki na yenye tija.

Hatua hii ya Manispaa ya Sumbawanga inatarajiwa kuongeza hamasa kwa wazazi, shule na wadau wa elimu kuendelea kushirikiana katika kuweka kipaumbele kwenye lishe shuleni kama nyenzo muhimu ya kujenga kizazi chenye afya bora, uwezo wa kufikiri na kiwango kizuri cha ufaulu.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Novemba 21, 2025, katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Lishe Kitaifa katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Ofisa Afya, Jesca Mwihava amewasisitiza wananchi kujenga utamaduni wa kula chakula bora na chenye virutubisho muhimu kwa afya.

Kwa upande wake, wakati akikabidhi unga wenye virutubisho kwa shule za sekondari, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga, Musa Musoma, amesema ni jukumu muhimu kwa kila shule kuhakikisha wanafunzi wanapata mlo kamili.

Amesema hatua hiyo si tu inaboresha afya za wanafunzi, bali pia inawasaidia kujenga tabia endelevu ya ulaji bora kuanzia wakiwa shuleni hadi kwenye familia zao.

Musoma ameongeza kuwa lishe bora shuleni ni nguzo muhimu katika kukuza uwezo wa mwanafunzi kufikiri, kuongeza umakini darasani, kupunguza magonjwa yatokanayo na lishe duni na hatimaye kuongeza kiwango cha ufaulu.

Pia, Musoma ameziomba shule, wazazi na jamii kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha programu za lishe shuleni zinakuwa endelevu na zenye matokeo chanya kwa watoto.

 “Lishe bora ni nguzo ya ufaulu wa mwanafunzi. Virutubisho vinavyopatikana kwenye mlo kamili humjenga kijana kiafya na kiakili, hivyo wazazi, walezi na uongozi wa shule wanapaswa kushirikiana kutekeleza ajenda ya mlo kamili bila kukoma,” amesema Musoma.

Kwa upande wao walimu wa shule za sekondari wamesema kuwa wanaendelea kutekeleza mpango wa mlo kamili shuleni kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula chenye ubora unaohitajika kwa afya na ufaulu.

Mwalimu Sadda Kibona kutoka Shule ya Sekondari Kizwite amesema kuwa upatikanaji wa chakula shuleni umebadilisha matokeo ya wanafunzi kwa kuwa wanakula shuleni.

“Baadhi ya wanafunzi walikuwa hawafiki shuleni kwa sababu za utoro na wengine kushindwa kufanya vizuri kutokana na ukosefu wa chakula bora, lakini kwa sasa wanafunzi wamebadilika hata uelewa wao uko tofauti na mwanzoni walipokuwa hawapati chakula.” amesema Kibona

Hata hivyo, baadhi wa wazazi na walezi kutoka maeneo tofauti ya Manispaa ya Sumbawanga wamekiri kuwepo kwa utofauti kwa watoto wao hasa kwenye ufaulu tangu zoezi la chakula lilipoanza.

Kwa ypande wao wanafunzi wa Shule ya Sekondari Sumbawanga akiwamo Moses Ludovick amesema kuwa wanafunzi wengi wamebadilika hasa kwenye masomo yao, uhudhuriaji darasani na ufaulu umeongezeka.

“Kutokana na upatikanaji wa chakula bora shuleni wanafunzi wengi wanahudhuria masomo tofauti na hapo nyuma ambapo kulikuwa na utoro na tabia ya uzembe kwa wanafunzi,” amesema Ludovick.

Aidha, Ofisa Lishe wa Manispaa ya Sumbawanga, Jesca Mwihava, amesema kuwa kiwango cha udumavu katika Manispaa hiyo kimefikia asilimia 34, hali ambayo bado ni changamoto kubwa licha ya mkoa wa Rukwa kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa chakula nchini.

 Amesema jitihada mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha kiwango hicho kinapungua kupitia programu endelevu za lishe katika jamii na shule.

Mwihava ameongeza kuwa Wiki ya Lishe Kitaifa ilianza Novemba 17 na leo, Novemba 21, ndiyo kilele chake, lakini juhudi za kutoa elimu hazitaishia hapa.

Amesema wataendelea kutoa hamasa na elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa lishe bora kuanzia ngazi ya familia, kwa lengo la kupambana na tatizo la udumavu na kuimarisha afya ya watoto na jamii kwa ujumla.