Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linachunguza chanzo cha moto ulioteketeza mabweni mawili ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Sumve iliyopo Wilayani Kwimba mkoani hapa.
Tukio hilo limetokea Alhamisi Novemba 20, 2025 saa 07:13 mchana baada ya moto uliozuka wakati wanafunzi wakiendelea na masomo darasani.
Moto huo uliteketeza mabweni ya Nkwame na Dk Magufuli ambayo yanatumiwa na wanafunzi wa shule hiyo kama makazi yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa katika taarifa yake kwa umma aliyoitoa leo Ijumaa Novemba 21, 2025, amesema hakuna mwanafunzi wala mtu mwingine aliyeripotiwa kujeruhiwa katika tukio hilo.
Hata hivyo, ajali hiyo imeacha simanzi kwa wanafunzi baada ya kuteketeza vifaa walivyokuwa wakitumia ikiwemo magodoro, nguo, na mali nyingine, huku chanzo cha tukio hilo kikiendelea kuchunguzwa.
“Moto ulienea kwa kasi kutokana na uwepo wa vifaa vinavyowaka haraka kama magodoro, nguo, mablanketi na mali nyingine za wanafunzi waliokuwa wakitumia mabweni hayo,” amesema Mutafungwa.
Amesema Jeshi la Polisi, Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na wananchi walifika eneo la tukio kwa haraka na kufanikiwa kudhibiti moto kabla haujasababisha madhara makubwa zaidi.
“Baadhi ya mali ziliokolewa ikiwamo magodoro, tranka, mablanketi, ndoo za maji na viatu,” imeeleza taarifa hiyo na kuongeza kuwa uchunguzi wa chanzo cha tukio hilo unaendelea, huku ulinzi ukiimarishwa katika shule hiyo na shule nyingine jirani.
“Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali, limeanza uchunguzi kuhusu tukio hilo la moto. Tunatoa wito kwa wananchi watoe ushirikiano kwa jeshi letu ili kufanikisha uchunguzi,” amesema Mutafungwa.

