Kibaha .Taasisi ya Peace Life for Persons with Disability Foundation (PLPDF) imezindua mradi wa Uwezo Wangu leo Ijumaa Novemba 22, 2025 mjini Kibaha, Mkoa wa Pwani, mradi unaolenga kuwawezesha zaidi ya wanawake na wasichana 100 wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika uongozi, maamuzi na maendeleo ya jamii.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mkurugenzi wa PLPDF, Sophia Mbeyela, amesema mradi huo unafadhiliwa na ADD International na utaanza kutekelezwa katika Wilaya za Kibaha na Bagamoyo, kwa kushirikiana na maofisa maendeleo wa maeneo hayo ili kuwafikia walengwa kwa wakati.
Mbeyela amesema kabla ya kuanza kwa utekelezaji, taasisi hiyo ilifanya utafiti ambao umebainisha changamoto zinazowazuia wanawake wenye ulemavu kushiriki katika michakato ya maamuzi na fursa za maendeleo, hivyo mradi umeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya kundi hilo.
Takwimu za Sensa ya Mwaka 2022 zinaonyesha kuwa Tanzania ina zaidi ya watu milioni 5.3 wenye ulemavu, sawa na asilimia 11.2 ya watu wenye umri wa miaka saba na kuendelea hali inayoonesha ukubwa wa kundi linalohitaji uwezeshaji na ushiriki mpana zaidi katika nafasi za kijamii na kiuchumi.
Wakili Gidion Mandesi amesema mradi huo utasaidia kuongeza uelewa kuhusu haki za watu wenye ulemavu, akibainisha kuwa ingawa kuna sheria nyingi zinazolinda kundi hilo, bado watu wengi hawajawahi kupata elimu ya kuzifahamu kwa undani.
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Albert Machua, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema serikali inaunga mkono mradi huo na itatoa ushirikiano ili kuhakikisha unatekelezwa kwa ufanisi.
Amesema maafisa ustawi wa jamii na watendaji wa halmashauri watashirikishwa kikamilifu ili kuwezesha mradi kufikia malengo yake.
Ester Mazoya mkazi wa Mkoa wa Pwani mwenye ulemavu wa miguu amesema kuwa ni vema mradi huo ukawafikia walengwa kwa wakati ili kuwasaidia kupata elimu na njia stahiki katika kufikia nalengo mahususi
Mradi wa Uwezo Wangu unatarajiwa kuwajengea uwezo wasichana na wanawake wenye ulemavu katika uongozi, kuwapa uelewa wa sera, kuwahamasisha kushiriki nafasi za maamuzi na kuongeza uwajibikaji wao katika shughuli za maendeleo ya jamii.
