Mwanza. Mvua iliyonyesha zaidi ya saa sita tangu saa 1 asubuhi leo Ijumaa Novemba 21, 2025 imewasababishia adha watumiaji wa njia inayokatisha daraja la Wakoma jijini Mwanza baada ya daraja hilo kufurika maji.
Huo ni mwendelezo wa maji kupita juu ya daraja hilo pindi Mto Mirongo unapojaa maji.
Baadhi ya barabara zilizoathirika ni ile ya U-turn na Uhuru ambazo zinapita juu ya Mto Mirongo.
Kutokana na mvua hiyo na madaraja kuzidiwa na kusababisha maji kupita juu yake, kumesababisha usumbufu kwa watumiaji wa maeneo hayo zikiwemo daladala, bajaji na watembea kwa miguu, ambapo baadhi ya vyombo hivyo vya usafiri vimelazimika kubadilisha ruti za safari zao.
Mwananchi imeshuhudia watembea kwa miguu wakipata taabu kupita katika eneo la daraja la Wakoma katika barabara ya Uhuru ambayo imejaa maji na tope kutokana na mvua hiyo.
Mmoja ya wananchi katika eneo hilo, Joseph Marwa amesema hali hiyo imekuwa ya kudumu kwa miaka mingi lakini mamlaka za Serikali zimekuwa hazichukui hatua zozote.
“Hili siyo jambo geni hapa kila mwaka mvua ikinyesha hali ni hii na mamlaka zinafahamu na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa, huwa wanasubiria tope likauke ndipo waje walitoe, hivyo tumezoea,” amesema Marwa.
Naye, Magdalena Sylvester ameiomba Serikali kuitazama kwa jicho pana changamoto hiyo kwakuhakikisha wanaliinua daraja la Wakoma ili maji yasipite juu na kuleta usumbufu.
Hata hivyo, mwaka 2022, Serikali iliahidi kujenga kingo za Mto Mirongo kwa kutenga zaidi ya Sh9.2 bilioni kujenga na kuimarisha kingo za mto huo unaokatisha katikati ya Jiji la Mwanza kuondoa adha ya mafuriko yanayotokea nyakati za masika na kuwaacha wakazi wa jiji hilo na kilio cha uharibifu na upotevu wa mali.
Mto Mirongo unaokusanya maji kutoka Wilaya za Magu, Kwimba na baadhi ya maeneo ya Wilaya za Nyamagana na Ilemela, humwaga maji yake ndani ya Ziwa Victoria na imekuwa ikifurika mara kwa mara kipindi cha masika huku maji yake yakisambaa na kusomba mali na bidhaa za wafanyabiashara katika mitaa ya Mabatini, Nera, Liberty na Uhuru jijini Mwanza.
Katika mafuriko hayo, maji ya mto huo pia hufurika hadi kupita juu ya daraja la Wamaasai katika barabara ya Uhuru na kukatisha mawasiliano kati ya barabara ya Uhuru, Liberty na Kenyatta.
Pamoja na kusomba bidhaa zinazowekwa nje ya maduka ya jumla na rejareja katika mitaa ya Nera na Liberty jijini Mwanza, mafuriko ya mto Mirongo pia husababisha mitaa kadhaa na barabara ya Uhuru kufungwa kutokana na maji kupita juu ya daraja la Wamaasai.