| Mkuu wa Chuo cha Bandari Dar es Salaam, Dkt. Lufunyo Hussein, akizungumza katika mahafali hayo, ambapo jumla ya Wahitimu 757 wamemaliza masomo yao. |
| Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa TPA, Bw. Mbarikiwa Masinga akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mkeli Mbossa kwenye mahafali hayo. |
MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa
Bandari Tanzania (TPA), Mhe. Balozi Ernest Mangu (IGP Mstaafu); ameipongeza Menejimenti ya TPA kwa uwekezaji mkubwa walioufanya katika Chuo cha Bandari Dar es
Salaam.
Mhe. Balozi Mangu ametoa
pongezi hizo jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwatunuku vyeti Wahitimu wa Mahafali ya 24 ya Chuo cha Bandari Dar es Salaam.
Alisema
TPA imekiwezesha chuo hicho kwa kufunga jumla ya mashine kumi (10) ‘simulator’ za kisasa ambazo zinatumika kufundisha masuala anuai, ikiwemo
mafunzo yanayohusisha uchimbaji wa mafuta na gesi.
“Natambua na kupongeza Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
Tanzania (TPA) kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika mwaka wa fedha 2024/2025 katika
chuo hasa kwa kuboresha mazingira ya utoaji mafunzo kwa kuongeza vifaa vya
kufundishia na kujifunzia.”
“…Mipango ya
Serikali ya kuendeleza Bandari za Dares Salaam, Bagamoyo, Tanga, Mtwara na zile
za maziwa pamoja na kufungamanisha Bandari Kavu, Reli na Barabara, itachochea
ukuaji wa biashara katika sekta hii kwa asilimia kati ya asilimia tano (5%)
hadi tisa (9%) kwa mwaka na kufungua fursa za ajira kati ya 80,000
hadi 120,000 za moja kwa moja na za muda katika kipindi cha miaka mitano
ijayo. Kwa wahitimu wa leo hii ni fursa kubwa kwani ajira hizi zinahusiana na
maarifa na ujuzi mlioupata kutoka katika Chuo hiki,” alisisitiza Mhe. Balozi Mangu ambaye alikuwa mgeni rasmi
katika mahafali hayo.
Awali akizungumza katika mahafali hayo, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mkeli Mbossa; Mkurugenzi Rasilimali
Watu na Utawala, Bw. Mbarikiwa Masinga alisema TPA chini ya Wizara ya Uchukuzi itaendelea kuimarisha
huduma za Chuo ziweze kuendana na mabadiliko mbalimbali ya Sera za Nchi.
| Moja ya mtambo wa kisasa wa kufundishia wanafunzi, ukioneshwa kwa mgeni rasmi kwenye sherehe za Mahafali ya Ishirini na Nne (24) ya Chuo cha Bandari Dar es Salaam. |
Aidha alibainisha kuwa uimarishaji wa sera ya
ushirikishwaji wa Sekta binafsi katika uendeshaji na uendelezaji wa Sekta ndogo
ya Bandari unafanywa ili kuendana na dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2050 na
mipango mingine ya Serikali ambayo inaonesha bayana umuhimu na upekee wa sekta
ndogo ya bandari katika uchumi, ajira na mapato ya nchi.
Aliongeza kuwa uboreshaji mafunzo yanayotolewa
na Chuo utawaongezea Wahitimu utaalamu na kujiamini katika kutafuta fursa za
ajira na katika majukumu yao mengine ikiwa ni pamoja na kutoa Rasilimali Watu yenye
sifa na Vigezo vinavyotakiwa katika utekelezaji wa shughuli za miradi mikubwa
ya kimkakati ya Serikali.
“…Napenda kurejea maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa siku ya uzinduzi wa Bandari Kavu
Kwala kwamba “ …..Maboresho ya
bandari nchini yaendane na maboresho ya Chuo cha Bandari…..”.
“Nitumie fursa kueleza kwamba mimi
binafsi pamoja na Menejimenti ya TPA ninayoiongoza, tutaendelea kufanya mageuzi
makubwa katika sekta ya bandari na pia kukiboresha Chuo cha Bandari kwa
kukipatia Miundombinu ya kisasa, vifaa na mitambo ya kufundishia, mifumo ya
TEHAMA, kuajiri watumishi wapya wenye sifa zinazotakiwa pamoja na kuendeleza waliopo
waendane na kasi ya mageuzi katika sekta,” inaeleza taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Mbossa.