WAKATI mashabiki wa Simba wakiendelea kununua tiketi ili kushuhudia pambano la kwanza la makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika la Jumapili dhidi ya Petro Atletico ya Angola, kocha wa kikosi hicho, Dimitar Pantev amegeuka mbogo akiwatega washambuliaji wa kati wa timu hiyo.
Simba ina washambuliaji watatu matata wakiongozwa na Jonathan Sowah, Steven Mukwala na Seleman Mwalimu ‘Gomez’ ambao yeyote au wawili wanaweza kuanzishwa katika pambano hilo la Kundi D lenye klabu za Esperance ya Tunisia na Stade Malien ya Mali.
Pantev, ambaye amepewa jukumu la kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika michuano hiyo ya CAF, amekuwa akifuatilia kwa karibu mwenendo wa safu ya ushambuliaji, ambayo hadi sasa bado haijatoa kile kinachotarajiwa na wengi japo timu imeonyesha maboresho maeneo mengine.
Katika mechi nane zilizochezwa msimu huu katika mashindano yote, watatu hao wa kati wamefunga mabao matatu tu. Katika idadi hiyo, Sowah ndiye anaongoza akiwa na mabao mawili katika Ligi Kuu Bara, huku Mwalimu akifunga bao moja.
Mukwala aliyepachika mabao 13 msimu uliopita akiwa na timu hiyo katika ligi, ndiye straika pekee ambaye bado hajafungua akaunti ya mabao msimu huu, huku mchezaji mwingine anayetumika kama mshambualiji wa Simba ni Kibu Denis.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya benchi la ufundi, Pantev amewacharukia washambuliaji hao na kuwataka kuongeza ukatili dhidi ya mabeki wa timu pinzani akiwaeleza mechi ya Jumapili inahitaji utulivu wa kutosha na ubunifu ndani ya eneo la hatari.
Chanzo kimoja cha ndani ya timu kilisema Pantev, aliwataka mastraika kujituma zaidi na kuchukulia kwa uzito kila nafasi ambayo itakuwa ikipatikana katika mechi hiyo ili kuwapa raha maelfu ya mashabiki wa Simba ambao watakuwa wamejitokeza siku hiyo kwa Mkapa.
Kwa upande wao, wachezaji wanaonekana kuelewa uzito wa kile walichoelezwa na Pantev. Sowah, ambaye ameanza kuonyesha makali yake katika mechi ya mwisho ya ligi na hata ile ya kirafiki dhidi ya JKT Tanzania, anatajwa kuwa mchangamfu zaidi mazoezini, akionekana kutaka kuendeleza kile alichofanya msimu uliopita akiwa na Singida Black Stars.
Sowah aliifungia Simba bao la ushindi dhidi ya JKT Tanzania katika mechi ya mwisho ya ligi wakati timu hiyo ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 kabla ya kutupia mbili katika mechi ya kirafiki dhidi ya maafande hao wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 6-0 wikiendi iliyopita.
“Niwe mkweli bado sijawa kwenye kile kiwango ninachohitaji, naamini kila kitu kitakuwa sawa na mashabiki wategemee mambo mazuri kutoka kwangu na timu kwa ujumla,” alisema Sowah.
Mukwala ambaye hajafunga, amekuwa akifuatiliwa kwa ukaribu na benchi la ufundi. Wapo wanaoamini kuwa akifunga bao moja tu, huenda mlango wa mabao ukafunguka na kuleta ushindani mkubwa ndani ya kikosi.