Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamangamba Kabudi amewataka waaandishi wa vitabu nchini kuongeza ubunifu katika uandishi na uchapaji wa vitabu ili kuongeza mvuto kwa wasomaji.
Amesema licha ya vitabu kuchangia kukuza uchumi, bado vitabu hivyo vimekuwa ni urithi adimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Profesa Kabudi ametoa wito huo leo Ijumaa Novemba 21, 2025 wakati akizindua maonyesho ya 32 ya Kitaifa ya Vitabu Tanzania, yaliyofanyika Maktaba Kuu ya Taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Kuu ya Taifa (Bohumata), Dk Mboni Ruzegea(kushoto) akifafanua jambo mbele Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamangamba Kabudi, baada ya kuzindua maonyesho ya 32 ya kitaifa ya Vitabu Tanzania. Picha na Hadija Jumanne
”Wataalamu wa masuala ya ubongo wanasema usiposoma kitabu, ubongo unasinyaa, sasa ili uendelee kuwa na uzee mzuri unatakiwa usome vizuri ili ubongo usisinyae” alisema Profesa Kabudi.
Pia amekemea tabia ya baadhi ya jamii kupotosha lugha ya Kiswahili kwa kubananga maneno na kuyafinyanga na hivyo kuharibu lugha ya Kiswahili.
“Tumeanza kukibananga Kiswahili, tumeanza kukifubaza na tunakididimiza Kiswahili chetu, wakati lugha ya Kiswahili imesheheni masihara na utani wenye utamu wake,” amesema Profesa Kabudi na kuongeza
”Siku hizi Kiswahili kimepoteza ladha, Kiswahili ni lugha ya masihara, ni lugha ya mzaha, ni lugha utani…leo hii vijana wengi wa Kitanzania wanazungumza Kiswahili ambacho hakina ladha, hakina masihara, hakina utamu, tunaachia maneno jinsi yalivyo na wakati mwingine tunapotosha kabisa lugha hii,” amesema Profesa Kabudi.
Hata hivyo, aliwataka waandishi wa vitabu nchini kutumia taaluma hiyo kurudishwa Kiswahili katika ladha yake, kulinda amani ya nchini, kulinda maadili na kulinda utu wa kila Mtanzania.
”Bodi ya Huduma za Maktaba Kuu ya Taifa ishirikiane na wadau wengine kukuza lugha ya kiswahili na pia wadau na waasisi na watafsiri wa lugha ya Kiswahili mtumie jukwaa hili la maonyesho kama fursa ya kujitangaza kidunia, kiutamaduni, kukuza ajira na kulinda amani ” amesema.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Kuu ya Taifa (Bohumata), Dk Mboni Ruzegea amesema vitabu ni hifadhi ya maarifa ya utamaduni, ambayo Tanzania inajibunia
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamangamba Kabudi, akikata utepe kuzindua maonyesho ya 32 ya kitaifa ya Vitabu Tanzania, yaliyofanyika Maktaba Kuu ya Taifa, Jijini Dar es Salam. Picha na Hadija Jumanne
“Kwa sasa bodi imeanza kununua vitabu kutoka kwa wachapishaji wa vitabu wa ndani na tuna mshukuru rais kwa kutenga fedha kwa ajili ya kununua vitabu hivyo,” amesema Dk Ruzegea.
Amesema wanaomba Wizara ya Habari, Utamduni, Sanaa na Michezo iendelee kuipa nguvu sekta ya vitabu ili iweze kufanya vizuri zaidi.
“Tuna amini bila vitabu wala sera imara hatuwezi kujenga uchumi imara,” ameongeza Dk Ruzegea.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji Tanzania (PATA), Hermes Damian amesema Maonyesho ni i fursa kwa Tanzania kujitangaza duniani.
“Kupitia maonyesho hayo tunayo mengi ya kujifunza kuhusu lugha ya Kiswahili,” amesema Damian.
Maonyesho hayo ya siku sita kuanzai leo hadi Novemba 26, 2025 yameandaliwa na PATA kwa kushirikiana na Bohumata na kauli mbiu yake ni ‘Vitabu ni hfadhi ya maarifa na utamaduni’.
