Dar es Salaam. Baadhi ya wanawake wa Kata ya Kigogo, Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, wameendelea kunufaika na mradi wa kuwajengea uwezo na uwezeshaji ili kujikwamua kiuchumi.
Mradi huo unaoendeshwa na taasisi isiyokuwa na kiserikali ya Women of Influence ambayo imejikita kuwajengea uwezo wanawake namna ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia, rushwa ya ngono sambamba na kuwawezesha kupata mitaji kupitia mikopo rafiki.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Doreen Kalugira ameliambia Mwananchi leo Ijumaa Novemba 21,2025 shirika hilo kujihusisha kuwasaidia wajasiriamali kukuza biashara zao, pia linawaunganisha fursa mbalimbali za kiuchumi.
“Taasisi hii imeendelea kuleta mageuzi makubwa kwa wanawake wajasiriamali wadogo nchini, kuwapa taarifa sahihi kuhusu mikopo rafiki isiyo na riba.
“Kuwasaidia kukamilisha vigezo vinavyohitajika na kuwajengea uwezo wa kibiashara. Pia, tunawaongoza katika taratibu za kisheria za kusajili biashara zao na kuwajengea uwezo namna ya kufanya biashara zao ili kupata faida,” amesema Kalugira.
Kwa mujibu wa Kalugira, mwezi huu taasisi hiyo inasherehekea mafanikio ya vikundi viwili vya Mkombozi na Nange vya Kigogo vilivyofanikiwa kupata mikopo ya Serikali isiyokuwa na riba ya Sh39.5 milioni.
“Women of Influence imewasaidia wanawake hawa kusajili makundi yao kupitia njia mbalimbali ikiwemo kuandaa, kujaza na kuwasilisha nyaraka muhimu za maombi ya mikopo, ikiwemo kuzithibitisha kisheria.
“Baada ya mikopo hiyo kuidhinishwa, taasisi inaendelea kuwaongoza vikundi hivyo hadi kupata cheti cha kulipa kodi na leseni za biashara, hatua muhimu katika kufanikisha uhalali wa biashara zao,” amesema.
Kalugira amefafanua kuwa juhudi hizo zimewezeshwa kwa msaada wa Women First International, taasisi ya Kimarekani inayounga mkono jitihada za kiuchumi za wanawake Tanzania.
Katika hatua nyingine, Kalugira amesema Women of Influence imebuni programu ya simu (mobile application) inayoitwa ‘Kilinge Digital’, inayowezesha kupata taarifa za pamoja kuhusu mikopo rafiki inayotolewa na taasisi mbalimbali za kifedha nchini.
“Lengo ni kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu mikopo, hasa kwa wanawake wanaofanya biashara ndogondogo na kubwa ambao mara nyingi wanakosa taarifa.
“Tunataka kuona wanawake wakipata mitaji inayowasaidia kuanzisha na kukuza biashara zao. Tukiwapa taarifa, ujuzi na mitaji rafiki, tunawasaidia kuinua familia zao na uchumi wa taifa,” ameeleza Kalugira.
Amefafanua kuwa Women of Influence sio tu inawezeshaji wa wanawake kuhusu mikopo, bali pia inawajengea misingi imara ya kibiashara na kiuchumi ili kuchochea kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya Kundi hilo katika jamii.
“Uwezeshaji wa kiuchumi unawapa wanawake sauti ya kuzungumza wanapokumbana na ukatili. Pia, wanawake wanapokuwa na uwezo wa kifedha, wanaweza kuwahudumia familia zao kwa mahitaji ya msingi na kuwasomesha watoto wao,” amesema.
Mjumbe wa kikundi cha Mkombozi, Sylvia Alphonce amesema mchakato wa kuomba mkopo wa Serikali una utaratibu mzuri lakini unachukua muda mrefu kutokana na changamoto mbalimbali, hata hivyo ameishukuru Kilinge cha Sheia kuwasaidia kufanikisha.
“Wametusaidia sana katika mchakato huu kwa kutusaidia kutusajilia kikundi, kuomba mkopo, kututengenezea nyaraka muhimu pamoja na kutusaidia kupata leseni na Tin namba ya kikundi,” amesema Sylvia.
