Wanawake waongoza kwa idadi wahitimu Rucu

Iringa. Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (RUCU) leo kimefanya mahafali yake ya 18 katika viwanja vya chuo hicho jijini Iringa, ambapo jumla ya wahitimu 1,658 wametunukiwa vyeti, stashahada, shahada na shahada za uzamili.

Katika mahafali hayo, wanawake wameongoza kwa idadi kubwa, ikiwa ni 920, dhidi ya wanaume 738, hatua inayotafsiriwa kama ishara ya ukuaji wa usawa wa kijinsia katika elimu ya juu nchini.

Mahafali hayo yameenda sambamba na mvua kubwa iliyonyesha alfajiri, jambo ambalo wengi wamelitafsiri kama baraka kwa safari mpya ya wahitimu hao.

Akizungumza katika mahafali hayo, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Chrispina Lekule amesema ongezeko la wahitimu wanawake linaonyesha mabadiliko chanya katika dhana ya usawa wa fursa za elimu.

Wahitimu wa kozi mbalimbali katika chuo kikuu Katoliki Ruaha kilichopo halmashauri ya Manispaa ya Iringa wakiwa katika shamrashamra za mahafali yao iliyofanyika Leo Novemba 21, 2025 katika viwanja vya RUCU. Picha na Christina Thobias



“RUCU inaendelea kutoa elimu ya ubunifu na yenye mwelekeo wa kulijenga taifa. Tunaamini wahitimu wetu hususan wanawakewatakuwa chachu ya mabadiliko katika jamii zao,” amesema Prof. Lekule.

Mgeni rasmi, Askofu wa Jimbo Katoliki la Njombe, Eusebio Kyando amewataka wahitimu kutoridhika na kiwango walichofikia, akisema elimu ni njia isiyokoma.

“Msiridhike na hatua hii. Endeleeni kujiongezea maarifa, kwani taifa linawategemea katika kuliletea mabadiliko,” amesema Askofu Kyando.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Linda Selekwa aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Iringa, amekipongeza chuo kwa kusisitiza ubunifu, utafiti na taaluma zenye kuleta suluhisho katika jamii. Amewataka wahitimu kutumia elimu kama “silaha” katika kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi.

Wahitimu wa kozi mbalimbali katika chuo kikuu Katoliki Ruaha kilichopo halmashauri ya Manispaa ya Iringa wakiwa katika shamrashamra za mahafali yao iliyofanyika Leo Novemba 21, 2025 katika viwanja vya RUCU. Picha na Christina Thobias



Sauti za wanawake wahitimu

Wahitimu wanawake walionekana wenye furaha na matumaini makubwa kuhusu mustakabali wao, huku kila mmoja akieleza namna atakavyotumia taaluma yake kuleta matokeo chanya kwenye jamii.

Anna Peter  aliyehitimu Shahada ya Uuguzi na Ukunga amesema, “Nimetoka kwenye familia ya kipato cha chini, lakini leo ninasimama kama mhitimu. Nitaitumia taaluma yangu kuelimisha akina mama kuhusu afya ya uzazi na kupunguza vifo vya mama na mtoto vijijini.”

Joyce Mwakasege aliyehitimu Shahada ya Sheria amesema “Rucu imenipa misingi ya uadilifu na haki. Nitapigania haki za wanawake na watoto kupitia taaluma yangu.”

 “Nia yangu ni kufungua biashara ndogondogo na kuwahamasisha wanawake kuwa wajasiriamali wenye kujitegemea.” Amesema Hadija Hassan aliyehitimu Stashahada ya Utawala wa Biashara.