Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mbeya, imewaachia huru washtakiwa watatu waliokuwa wameshtakiwa kwa kosa la mauaji ya mwanakijiji mwenzao, baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha kesi hiyo dhidi yao.
Walioachiwa huru ni Fadhili Mashambwa, Sebastian Juma na Maneno Lemsi ambao walishtakiwa kwa kosa la mauaji ya Yohana Shonza, kinyume na kifungu cha cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Jaji Musa Pomo alitoa hukumu hiyo Novemba 17, 2025, na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Pomo aliwaachia huru washtakiwa wote watatu na kueleza kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi hiyo dhidi ya washtakiwa hao ambapo katika kesi hiyo ilitegemea zaidi ushahidi wa kimazingira.
Mauaji hayo yalidaiwa kutokea Desemba 10, 2023 katika kitongoji cha Idenderuka, Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya.
Katika kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi sita, kielelezo kimoja (maelezo ya onyo), huku washtakiwa hao wakitoa ushahidi wao wenyewe bila kuita mashahidi wengine.
Shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Kassim Khalid ambaye alikuwa kiongozi wa kitongoji hicho, alidai Desemba 11, 2023 alipigiwa simu na msamaria mwema akimweleza kuwa kuna mtu amelala kando ya barabara akiwa anavuja damu.
Alidai alipofika alimkuta Yohana ameshafariki huku akiwa na jeraha kichwani na kwenye bega la kushoto ambapo polisi walifika eneo hilo wakiwa wameongozana na daktari ambaye aliufanyia uchunguzi mwili huo na kubaini chanzo cha kifo hicho ni kutokwa na damu nyingi.
Alidai Desemba 14, 2023 alipata taarifa kutoka kwa ndugu wa marehemu wakidai waliohusika na mauaji hayo ni washtakiwa hao watatu, ambapo ndugu hao walieleza kuwa mshtakiwa wa tatu anatuhumiwa kwa sababu kumekuwa na madai kuwa marehemu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wa mshtakiwa.
Alidai kuwa Fadhili, alihusishwa na mauaji hayo kwa sababu alikuwepo kwenye kikao ambacho Yohana aliwaambia wanafamilia yake kuwa akifariki asizikwe na sarafu iliyokuwa mwilini kwake katika mkono wa kushoto.
Alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa wa kwanza, aliyekuwa akijihusisha na ununuzi na uuzaji wa sarafu ambapo inadaiwa alimtafuta rafiki yake (mshtakiwa wa pili) ili kwa pamoja waweze kupata sarafu hiyo kutoka kwa marehemu.
Baada ya kusikia madai hayo, shahidi huyo alidai kuwajulisha polisi, ambapo kwa kushirikiana na mgambo walifanikiwa kuwakamata washtakiwa wote watatu Desemba 19, 2023.
Shahidi wa pili, Benson Shonza, alidai Maneno alimuua Yohana kutokana na mgogoro wa mapenzi uliomhusisha mwanamke aitwaye Melisia Samuel au Mwanne (shahidi wa nne wa Jamhuri).
Alidai kuwa kabla Yohana hajafariki, aliwaambia mbele ya mshitakiwa wa kwanza kuwa alikuwa na sarafu katika mkono wake wa kushoto, ambapo walikuja kumshuku mshtakiwa huyo kuhusika na mauaji hayo kutokana na mshtakiwa huyo kufanya biashara ya kuuza sarafu.
Akihojiwa na upande wa utetezi, alieleza kuwa hakuwa na ushahidi kwamba marehemu alikuwa na sarafu mwilini kwake, ilikuwa ni kauli tu aliyoitoa na kuwa tuhuma za kumhusisha mshtakiwa wa tatu katika mauaji hayo zilitokana na mgogoro wa penzi lililomhusisha shahidi wa nne.
Shahidi wa nne, alithibitisha kuwa mshtakiwa wa tatu ni mumewe ambaye walifunga naye ndoa mwaka 2012 na kupeana talaka mwaka 2021.
Alidai baada ya kuachana na mumewe, alianza mahusiano na Yohana (marehemu kwa sasa ) mwaka 2022, na kuwa hakufahamu iwapo Maneno alikuwa anafahamu kuhusu uhusiano wake na Yohana.
Akihojiwa na upande wa utetezi shahidi huyo alidai katika maelezo aliyoandika polisi aliandika hajawahi kuwa na uhusiano na Yohana na hajui nani alihusika na mauaji hayo.
Shahidi wa sita, Koplo Humphrey alidai kumhoji mshtakiwa wa pili (Sebastian) na kuwa baada ya kukamilisha mahojiano hayo mshtakiwa alisaini kwa kutumia kidole gumba cha mkono wa kulia, kwani alijifahamisha kuwa hajui kusoma wala kuandika.
Nakala hiyo ya hukumu inaeleza kuwa, shahidi huyo aliporuhusiwa kumtambua mshtakiwa huyo,awali alielekeza kwa mshtakiwa wa kwanza na alipopewa nafasi mara ya pili alikosea pia ambapo alimtambua mshtakiwa wa tatu (Maneno) kuwa ndiye Sebastian.
Katika utetezi wao,mshtakiwa wa kwanza (Fadhili), alidai Disemba 10,2023 aliamka asubuhi na kwenda shambani kulima kisha akarudi saa sita mchana na kuwa Disemba 19, alikamatwa na kuwekwa kizuizini kwa muda wa wiki tatu kabla ya kusoemwa shtaka la mauaji.
Alidai kuwa Januari 15, 2024, alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Chunya, ambako alisomewa shtaka la mauaji ya Yohana Shonza na kusema hafahamu chochote kuhusu mauaji hayo na kueleza kuwa ni uzushi na kukana kushirikiana na washtakiwa wenzake kumuua Yohana.
Fadhili alidai kuwa hakuna ushahidi uliotolewa dhidi yake mbali na tuhuma tu,huku akikana kujihusisha na biashara ya sarafu pamoja na kukana madai kuwa alihudhuria kikao ambacho Yohana alieleza kuwa alikuwa na sarafu ndani ya mwili wake na kuomba mahakama imuachie huru.
Mshtakiwa wa pili, Sebastian, alidai Disemba 19, 2023 akiwa nyumbani kwake mgambo alimfuata na kumtaka kufika ofisi ya kijiji ambapo alipofika alipelejwa Kituo cha Polisi Chunya na kukaa mahabusu hadi Januari 15,2024,alipofikishwa mahakamani na kudai hajui lolote kuhusu mauaji hayo.
Aliiambia mahakama kuwa siku mauaji hayo yanadaiwa kutokea hakuwepo katika Kitongoji hicho na kuwa alikuwa amesafiri kuanzia Disemba 6, 2023 kwenda kwenye kijiji cha Lwanjilo kutafuta kuku kwa ajili ya biashara na kuwa alirejea Disemba 14,2023.
Alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa wa kwanza siyo rafiki yake bali ni mkazi mwenzake katika kitongoji cha Idendeluka huku akikana kuwahi kuandika maelezo yoyote ya onyo polisi ambapo alipoonyeshwa maelezo ya onyo aliyodaiwa kutoa yeye aliyakana na kueleza kuwa anajua kusoma na kuandika.
Mshtakiwa huyo aliieleza mahakama kuwa shahidi wa sita alishindwa kumtambua kwa usahihi mtu ambaye alidai kuwa aliandika maelezo yake (ambaye ni anadaiwa ni yeye) na kuomba mahakama kumuachia huru.
Mshtakiwa wa tatu alidai Disemba 19, 2023 akiwa shambani alikutana na mgambo aliyemweleza kuwa anahitajia katika ofisi za Kijiji na alipomuuliza kuna nini alimweleza kuwa atajua akifika huko,ambapo baada ya kufika alipelekwa kituo cha polisi na kukaa hadi Januari 15,2023 alipopelekwa mahakamani na kusomewa shtaka la mauaji.
Alidai kuwa shahidi wa nne,aliachana naye tangu mwaka 2021 ambapo baada ya kupeana talaka hakuwahi kuwa na mawasiliano naye na hakuwa anafahamu kama alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na Yohana (marehemu kwa sasa),huku akiomba kuachiwa huru na mahakama kwani kesi hiyo ni ya uzushi.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Pomo alieleza kuwa katika kesi za jinai upande wa Jamhuri una wajibu wa kuthibitisha kesi pasipo kuacha shaka,ambapo kesi hiyo ilitegemea zaidi ushahidi wa kimazingira.
Amesema suala ambalo Mahakama itaamua ni iwapo upande wa mashtaka umethibitisha, pasipo shaka yoyote kwamba washtakiwa wanahusika na mauaji ya marehemu.
Kuhusu ushahidi wa maelezo ya onyo yaliyodaiwa kuwa ni ya mshtakiwa wa pili, amesema anaona washtakiwa wenzake hawawezi kuhukumikwa kwa msingi tu wa ungamo lililotolewa na mshtakiwa mwenzao isipokuwa maelezo hayo yamethibitishwa na ushahidi mwingine.
Jaji Pomo amesema shahidi wa sita wa Jamhuri alishindwa kumtambua mtu ambaye aliandika maelezo yake na kuwa kwa kuzingatia mazingira hayo anona kwamba kuna uwezekano kwamba shahidi huyo alihoji mtu mwingine na kurekodi taarifa hiyo, na sio mshtakiwa wa pili.
“Zaidi ya hayo, maelezo yanayodaiwa kuwa ya mshtakiwa wa pili yalionyesha kuwa hajui kusoma wala kuandika. Hata hivyo, mahakamani hapo, mshtakiwa wa pili aliweza kusoma kwa sauti sehemu za maelezo hayo,” amesema Jaji.
Jaji Pomo amehitimisha kuwa Mahakama imeona upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi yake bila shaka dhidi ya washtakiwa hivyo kuwaachia huru washtakiwa wote watatu.
