Wawili mbaroni wakidaiwa kuhamasisha vurugu

Arusha. Jeshi la Polisi mkoani Arusha, limesema linawashikilia vijana wawili kwa tuhuma za kuongoza kundi sogozi la kueneza chuki kwa jamii.

Vijana hao ni Edwin Mboro na Victor Ndibalema ambao pia wanadaiwa kuhamasisha vurugu nchini wakishirikiana na wahalifu wengine.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha, Justine Masejo, leo Ijumaa Novemba 21, 2025, imedai kuwa uchunguzi wa tukio hilo unakamilishwa ili hatua nyingine za kisheria zifuate.

Jeshi la Polisi limesema watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti na kuwa linaendelea kuwahoji vijana hao.

“Jeshi la Polisi Arusha linapenda kutoa ufafanuzi juu ya picha mjongeo zinazoonekana katika baadhi ya mitandao ya kijamii zikieleza kuwa kuna vijana wawili wametekwa jijini Arusha,” imesema na kuongeza;

“Taarifa sahihi ni kwamba kwa nyakati tofauti tuliwakamata na tunaendelea kuwahoji vijana hao ambao ni Edwin (mkazi wa Sanawari) na Victor (mkazi wa Kijenge), kwa  tuhuma za kuongoza kundi sogozi la kueneza chuki kwa jamii na kuhamasisha vurugu nchini wakisshirikiana na wahalifu wengine.”

Kamanda Masejo ameeleza kuwa uchunguzi wa tukio hilo unakamilishwa ili hatua nyingine za kisheria zifuate.