Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuwa, kisonono ambao ni ugonjwa wa zinaa, kinazidi kuwa sugu kwa dawa za antibiotiki.
Taarifa iliyochapishwa Novemba 19, 2025 kwenye tovuti ya WHO imesema tahadhari hiyo inatokana na takwimu mpya kutoka mpango wake wa Ufuatiliaji wa Uongezekaji wa Uhimilivu wa Vijidudu vya Kisonono (EGASP), unaofuatilia kuenea kwa usugu wa dawa za ugonjwa huo.
Ripoti hiyo inaonyesha uwapo wa haja ya kuimarisha ufuatiliaji, kuboresha uwezo wa uchunguzi na kuhakikisha upatikanaji sawa wa matibabu mapya ya magonjwa ya zinaa (STI).
Utoaji wa takwimu hizi mpya umeendana na wiki ya uhamasishaji kuhusu usugu wa dawa dhidi ya vimelea vya magonjwa (AMR), jambo linalosisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za kimataifa dhidi ya usugu huo ambao hutokea wakati vijidudu vinapokuza uwezo wa kushinda dawa zilizoundwa kuviua.
Mpango wa EGASP ulioanzishwa na WHO mwaka 2015, hukusanya takwimu za maabara na kliniki kutoka vituo maalumu duniani kote ili kufuatilia usugu wa dawa na kuongoza miongozo ya tiba.
“Juhudi hizi za kimataifa ni muhimu katika kufuatilia, kuzuia na kukabiliana na usugu wa dawa za kisonono na kulinda afya ya umma duniani,” amesema Dk Tereza Kasaeva, Mkurugenzi wa Idara ya WHO ya Ukimwi, kifua kikuu, homa ya ini na magonjwa ya zinaa.
“WHO inaziomba nchi zote kushughulikia ongezeko la maambukizi ya magonjwa ya zinaa na kuingiza ufuatiliaji wa kisonono katika programu zao za kitaifa za STI,” amesema.
Wakizungumza na Mwananchi, wataalamu nchini Tanzania wanasema usugu wa dawa ni tatizo kubwa ambalo limekuwa likiongezeka.
Mfamasia na Mkufunzi wa shule ya famasia Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), David Mnyemba amesema magonjwa yaliyokuwa rahisi kutibika, kama vile kisonono na mengine, sasa yamekuwa yanasumbua kwenye matibabu.
“Tafiti nyingi tulizofanya ni kuonyesha extant (hali iliyopo hadi leo) ya usugu wa antibiotiki kwenye vituo mbalimbali vya kutoa huduma za afya nchini na mambo yanayosababisha,” amesema na kuongeza:
“Pia aina za magonjwa ambayo yameonyesha usugu zaidi. Kuhusu kisonono matokeo yanaonyesha kuwa rate (kiwango) inaongezeka, kuna tafiti zaidi zinakuja zenye takwimu halisi.”
Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi amesema nchini Tanzania antibiotiki zinazotibu kisonono zilijenga usugu na walifanya uamuzi wa kubadili dawa ambazo nazo kwa sasa zina usugu.
“Tulibadilisha dawa zilizokuwa zinatibu wakati huo, Penicillin zilishindwa kutibu kwa sasa tunatumia dawa zingine Cepritasol nazo zinagoma, kwa baadhi ya watu kuna mabadiliko yanatokea,” amesema.
Alipoulizwa hatua zipi nchi imechukua, Msasi amesema mara nyingi hatua haichukuliwi kwa ugonjwa mmoja mmoja kutokana na tatizo la usugu wa dawa kukumba magonjwa mengi.
“Tunachukua hatua kwa ujumla za kupambana na Uvida (usugu wa dawa) tunahusisha elimu, baadhi ya dawa kuziweka kwenye category (kundi) ambazo zinapatikana kirahisi tunaendelea kuhuisha. Kuna vitu vingi vinaendelea kinachotukwamisha ni tabia ya mtu kununua dawa bila ushauri wa daktari,” amesema.
Mpango wa EGASP unafuatilia usugu wa vimelea vya Neisseria gonorrhoeae dhidi ya dawa mbalimbali ili kuongoza uboreshaji wa matibabu. Unaendana na mpango wa AMR na Mfumo wa Ufuatiliaji wa Matumizi na Usugu wa Antibiotiki wa WHO (GLASS), ukitoa takwimu zenye uthibitisho wa ubora kwa ajili ya kuongoza miongozo ya kimataifa na kitaifa.
Ripoti ya kwanza ya EGASP (takwimu za 2015–2022) ilihusisha nchi nne pekee, ilhali ripoti ya mwaka 2024 (takwimu za 2023) ziliongezeka nchi tisa.
Inaonyesha uwepo wa ongezeko la usugu kwa dawa muhimu kama ceftriaxone na azithromycin.
EGASP hufanya kazi kupitia vituo maalumu vya ufuatiliaji kwa ushirikiano wa kiufundi wa WHO na kujenga uwezo wa kitaifa katika ufuatiliaji wa magonjwa ya zinaa na uimarishaji wa maabara.
Takwimu hizi zinajumuisha taarifa za kidemografia, kitabibu na viwango vya usugu wa dawa.
Kati ya mwaka 2022 na 2024, usugu kwa ceftriaxone na cefixime (antibiotiki kuu za kutibu kisonono) uliongezeka kwa kasi kutoka asilimia 0.8 hadi tano na kutoka ailimia 1.7 hadi 11 mtawalia, huku aina sugu zikiripotiwa katika nchi zaidi.
Usugu kwa azithromycin ulisalia kuwa asilimia nne, huku usugu kwa ciprofloxacin ukifikia asilimia 95. Ripoti inaeleza Cambodia na Vietnam ndizo ziliripoti viwango vya juu zaidi vya usugu.
Mwaka 2024, nchi 12 wanachama wa EGASP kutoka kanda tano za WHO ziliwasilisha takwimu, ongezeko kutoka nchi nne tu mwaka 2022.
Kwa mujibu wa WHO, hii ni hatua chanya inayodhihirisha kujitolea zaidi kufuatilia na kudhibiti maambukizi sugu ya dawa katika nchi na kanda.
Nchi hizo ni Brazil, Cambodia, India, Indonesia, Malawi, Ufilipino, Qatar, Afrika Kusini, Sweden, Thailand, Uganda na Vietnam ziliripoti jumla ya wagonjwa 3,615 wa kisonono.
Umri wa wastani wa wagonjwa ulikuwa miaka 27 (kuanzia 12 hadi 94). Kati ya wagonjwa hao, asilimia 20 walikuwa wanaume wanaojihusisha na ngono na wanaume na asilimia 42 waliripoti kuwa na wapenzi wengi ndani ya siku 30 zilizopita, huku asilimia nane waliripoti kutumia antibiotiki karibuni na asilimia 19 walisafiri hivi karibuni.
Mwaka 2024, WHO ilifanya ufuatiliaji wa vinasaba kwa kupima sampuli 3,000 kutoka nchi nane.
Tafiti za matibabu mapya kama zoliflodacin na gepotidacin na za usugu kwa tetracycline, zilifanywa na kituo cha WHO kwa kushirikiana na kingine cha usugu wa dawa kwa STI nchini Sweden, kwa uratibu na WHO.
Tafiti hizi zinasaidia kuongoza mikakati ya kudhibiti kisonono na uzuiaji kwa kutumia doxycycline (DoxyPEP).
Licha ya maendeleo makubwa, EGASP inakabiliwa na changamoto, zikiwamo ufadhili mdogo, utoaji taarifa usiokamilika na upungufu wa takwimu za wanawake.
WHO inatoa wito wa uwekezaji wa haraka, hususani katika mifumo ya kitaifa ya ufuatiliaji ili kuendeleza na kupanua ufuatiliaji wa usugu wa dawa kwa kisonono duniani.
