Winga Yanga awavujishia Simba faili la Waangola

SIMBA ipo katika maandalizi ya mwisho ya kukutana na Petro Atletico ya Angola katika mechi ya Kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini sasa kuna winga mmoja wa Yanga amewashtua juu ya wapinzani wao hao.

Simba itavaana na Petro  Atletico kuanzia saa 10:00 jioni kabla ya baadaye kusafiri kuifuata Stade Malien ya Mali wiki ijayo na kusubiri hadi Februri mwakani kuvaana na Esperance ya Tunisia waliyopangwa nao kundi moja kusaka tiketi ya kutinga robo fainali.

Sasa wakati Simba ikiingia kambini tayari kwa maandalizi ya pambano hilo la kwanza la makundi, winga wa zamani wa Yanga, Mahaltse Makudubela ‘Skudu’ ambaye anacheza soka Angola akiitumikia Wiliete Benguela iliyomzingua kwa kutomtengenezea kibali cha kazi na kumsababisha kurejeshwa kwao Afrika Kusini, ndiye aliyeamua kuiuma sikio Simba mapema.

Akizungumza na Mwanaspoti, Skudu alisema Simba inatakiwa kujipanga vyema kwani itakutana na mpinzani mgumu licha ya ubora na rekodi za Wekundu hao wakiwa nyumbani.

WAANG 03

Skudu alisema, Simba inatakiwa kujipanga na mambo mawili ambapo kwanza ubora mkubwa wa Petro upo eneo la kati ambapo wana viungo bora wanaojua kutengeneza nafasi.

Winga huyo wa zamani wa Marumo Gallants, alisema eneo la hilo la kati viungo wa kati wanajua kupiga pasi za maana na kukimbia haraka, huku watu wengine hatari ni viungo washambuliaji wa pembeni ambao ni mafundi sana.

“Wana viungo wazuri sana Petro, najua Simba ina rekodi nzuri nyumbani, lakini wasiwakadirie Petro ni timu nzuri. Pale kati wana viungo wanaojua sana kupiga pasi za haraka,” alisema Skudu ambaye aliwahi kuitumikia Yanga kwa msimu mmoja.

WAANGOLA

“Ukiacha viungo hao kuna mawinga wao nao ni wazuri sana wana ufundi sana wa kujua kupenya na kuwapunguza mabeki na kutengeneza nafasi,” aliongeza nyota huyo aliyeitumikia pia AS Vita kabla ya kukimbilia Wiliete iliyotolewa na Yanga katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa.

Pia Skudu aliongeza kwa kufichua kuwa, ukuta wa Simba utakutana na kipimo kigumu kwani Petro ina washambuliaji wazuri ambao kama wakifanya makosa wanaweza kuwaadhibu.

WAANG 04

“Sisi walitufunga tulipokutana nao, eneo jingine ambalo Simba wanatakiwa kuwa imara ni katika safu yao ya ulinzi, Petro wana washambuliaji wazuri sana wana nguvu na akili ya kufunga.|”

Hata hivyo, Skudu aliongeza bado anaamini Simba ina akili ya kujua kucheza mechi za kimataifa kwa hesabu hususani zile za nyumbani.

WAANG 02

Rekodi zinaonyesha kuwa katika mechi za msimu uliopita, Simba haikupoteza mechi yoyote nyumbani zaidi ya kutoka sare ya 1-1 na RS Berkane ya Morocco katika fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku mbili za msimu huu hatua za awali ikitoa sare dhidi ya Gaborone United ya Botswana na Nsingizini Hotspurs ya Eswatini.