Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, ameibuka na kuweka wazi kuhusu uvumi unaosambazwa katika mitandao ya kijamii kwamba anaumiliki kampuni ya mabasi ya Ester. Akiwahutubia mamia ya wananchi katika viwanja vya Bombadia, Manispaa ya Singida, Novemba 21, 2025, Dk. Mwigulu amesema taarifa hizo ni za uongo na zimekuwa zikienezwa bila uchunguzi wowote.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa hawana hofu ya kutunga au kusambaza taarifa zisizo na ukweli, bila hata kufanya utafiti mdogo kuhusu mtu anayehusishwa.
“Juzi juzi nikasikia tumechoma magari ya Ester ya mbunge wa Iramba Magharibi, eti ni mali ya mke wangu. Magari haya yanaitwa Ester kwa sababu mmiliki ameyaita kwa jina la mke wake. Mke wangu mimi haitwi Ester, anaitwa Neema,” alisema.
Akiendelea kufafanua, Dk. Mwigulu alikanusha fununu kwamba mabasi hayo yanaweza kuwa ya mama yake, akisema:
“Mama yangu ni binti wa Kiislamu anaitwa Asha Ramadhani Mohamed.”
Dk. Mwigulu ameweka wazi pia kuwa anatoka katika familia ya kifugaji ambayo haijihusishi na biashara kama za miwa, na kwamba hajawahi kuwekeza kwenye biashara yoyote ya aina hiyo.
“Nimeingia serikalini na uwekezaji mkubwa ninaoufanya ni kuwasomesha watoto. Nina zaidi ya watoto 500 ninaowasomesha; nimewekeza kwenye huduma za watu, sio biashara,” alisisitiza.
Ametumia nafasi hiyo kuwaasa Watanzania kutokubali kila taarifa wanazopewa bila kufanya uhakiki, huku akisisitiza umuhimu wa kuenzi amani na ukweli.
