KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kutupa karata ya kwanza ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco, huku mashabiki wa klabu hiyo wakiwa na presha zaidi na eneo la ushambuliaji, lakini kuna nyota mmoja amewatoa hofu mapema.
Celestine Ecua aliyesajiliwa na Yanga msimu huu kutoka Ivory Coast amejivisha mabomu na kuwatoa hofu mashabiki hao kwa kuwaambia kwamba anaamini kuna sapraizi kubwa ambayo Waarabu watakutana nayo visiwani Zanzibar, huku mwenyewe akisisitiza anaitaka mechi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ecua alisema mechi ya leo dhidi ya AS FAR Rabat itakayopigwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan, licha ya kuwa ni mechi ngumu, anaomba apate muda wa kutosha ili awafurahishe mashabiki wa Yanga.
Ecua alisema, anajiona bado ana deni kubwa mbele ya mashabiki wa Yanga na hataki moto wake upotee kuanzia lile bao la Mtibwa, na atayafanya hayo kama kocha wake Pedro Goncalves atampa muda wa kutosha kwani anataka kuwazima Waarabu hao.
“Tuna mechi ngumu kweli, tunaiheshimu FAR Rabat ni timu nzuri, lakini Yanga tupo nyumbani mashabiki wetu wasiogope waje uwanjani kwa wingi kutupa nguvu kwani kuna sapraizi yao, tupo nyumbani na naamini tutatumia vyema dakika 90. Natamani sana kucheza hii mechi,” alisema.
“Unajua tangu nimefunga lile bao kwenye mechi ya ligi kuna nguvu imenijia kwamba kama nitapata muda wa kutosha zaidi hata kwenye mechi hii nitawafurahisha mashabiki wetu. Mimi sioni kama tuna safu mbovu ya ushambuliaji, nikiamini hivyo itakuwa mimi na wenzangu hatufai na sio ukweli, ni suala la utulivu, tuna kocha mzuri ninachoomba ni kupata muda wa kutosha wa kucheza na mashabiki watafurahi,” alisisitiza Ecua, nyota wa kimataifa wa timu ya taifa ya Chad.
Ecua alisema ameanza kuzoea ugumu wa mechi za ligi ya ndani, lakini hana shida na mechi za kimataifa ambazo amekuwa akizicheza tangu akiwa ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
“Siogopi hizi mechi za CAF, nimecheza tangu nikiwa Asec kitu muhimu mashabiki wetu waje uwanjani, watupe nguvu ili wapinzani wetu wajue wanakutana na timu kubwa hapa Afrika.”
Ikumbukwe katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar, Ecua alipiga bao moja lililowakosha mashabiki wengi wakati Yanga ikishinda mabao 2-0 na kuvuna pointi tatu muhimu zilizowafanya kwa sasa kuongoza msimamo wakiwa na pointi nne baada ya kushuka uwanjani mara nne.