RAUNDI ya sita ya Ligi ya Championship inaendelea tena wikiendi hii kwa mechi tatu kupigwa leo Jumamosi na nyingine tatu kesho Jumapili za kuhitimisha, huku vita kali inayosubiriwa ni kati ya Kagera Sugar na Polisi Tanzania.
Mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba mkoani Kagera inarudisha kumbukumbu ya timu hizo mara ya mwisho zilipokutana msimu wa 2022-2023 zikiwa katika Ligi Kuu Bara kabla ya kushuka daraja na kushiriki Ligi ya Championship.
Kagera iliyodumu katika Ligi Kuu Bara kwa miaka 20 tangu ilipoanza kushiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kushinda mechi tano tu, sare minane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15, kufuatia kukusanya pointi zake 23.
Timu hiyo inayonolewa na aliyekuwa nyota wa Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, Juma Kaseja aliyewahi kuitumikia pia Kagera akiwa mchezaji na kocha wa makipa, ana kazi ya kukipambania kikosi hicho ili kirejee tena katika Ligi Kuu Bara.
Kwa upande wa Polisi Tanzania, msimu wa 2024-2025, haukuwa mzuri baada ya kumaliza ikiwa nafasi ya 10, katika Ligi ya Championship na pointi 33, kufuatia kushinda mechi nane tu, sare tisa na kupoteza 13, ikifunga mabao 44 na kuruhusu 33.
Kikosi hicho kinapambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, kilipomaliza nafasi ya 15 na pointi zake 25, kufuatia kushinda mechi sita tu, sare saba na kupoteza 17, kikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.
Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana kwenye Uwanja wa Kaitaba, ilikuwa katika Ligi Kuu ambapo Kagera ilishinda mabao 2-0, yaliyofungwa na waliokuwa nyota wa kikosi hicho, Abdulaziz Makame na Mbaraka Yusuph, mechi ikipigwa Oktoba 8, 2022.
Kagera inaingia katika mechi hiyo ikiwa na morali kubwa baada ya kuifunga Stand United ‘Chama la Wana’ mabao 4-0, kwenye Uwanja wa Kaitaba wiki iliyopita, huku kwa upande wa Polisi ikitoka sare ya kufungana bao 1-1, dhidi ya timu ya Bigman.
Mechi nyingine itapigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, ambapo African Sports iliyoshuka daraja msimu wa 2015-2016, itakuwa na kibarua cha kupambana na Geita Gold inayosaka tiketi ya kurejea Ligi Kuu baada ya kushuka 2023-2024.
Sports itahitaji kurudisha morali kwa wachezaji wa kikosi hicho baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo, ikichapwa mabao 4-1 na Kagera Sugar kisha 2-1 na Mbeya Kwanza, huku kwa Geita Gold ikitoka kuifunga Gunners 3-0, wiki iliyopita.
Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, TMA iliyochapwa wiki iliyopita nyumbani bao 1-0, dhidi ya maafande wa Transit Camp, itaikaribisha Songea United iliyoifunga B19 zamani Tanesco mabao 4-2, ikiwa ni mechi ya mwisho kwa leo.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho Jumapili kwa mechi tatu, ambapo KenGold iliyoifunga Hausung mabao 3-1, itakuwa kwenye Uwanja wa Manispaa ya Chunya jijini Mbeya kuikaribisha Mbuni ya Arusha iliyoichapa Barberian zamani Kiluvya United 3-0.
Baada ya msimu bora wa 2023-2024, mashabiki na wapenzi wa soka hususani wa Jijini Mbeya walitarajia KenGold ingeendeleza ilichokifanya katika Ligi ya Championship, japo baada ya kupanda daraja mambo yalikuwa ni tofauti na kurejea ilipotoka.
Kwa msimu wa 2023-2024, KenGold ilitwaa ubingwa wa Championship, ikiibuka kinara na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji ya Mwanza iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 67, iliyorejea Ligi Kuu baada ya miaka 21 tangu iliposhuka mwaka 2001.
Licha ya kiwango bora, lakini msimu wa 2024-2025, KenGold ilishindwa kumudu presha za Ligi Kuu na kuburuza mkiani na pointi 16 ikishinda mechi tatu tu ikitoka sare saba na kupoteza 20, ikiungana na Kagera Sugar iliyomaliza ya 15 na pointi 23.
B19 zamani Tanesco iliyochapwa mechi zote tano mfululizo ilizocheza hadi sasa, itakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro kucheza dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’, yenye kumbukumbu ya kutoka kuchapwa kwa mabao 4-0, dhidi ya Kagera Sugar.
Stand iliyoshuka daraja msimu wa 2018-2019, ilimaliza nafasi ya 19 na pointi 44, baada ya kushinda mechi 12, sare minane na kupoteza 18, ikifunga mabao 38 na kuruhusu 50, ambapo msimu huu imeanza vibaya kutokana na changamoto kubwa za ukata.
Msimu uliopita, Stand ilimaliza ikiwa nafasi ya tatu na pointi 61, ambapo ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara, ikianza kwa kuiondosha Geita Gold iliyomaliza ya nne na pointi 56, katika Ligi ya Championship kwa jumla ya mabao 4-2.
Baada ya Stand kuitoa Geita Gold ikacheza mtoano nyingine na Fountain Gate iliyotolewa pia hatua hiyo na maafande wa Tanzania Prisons kwa jumla ya mabao 4-2, ambapo kikosi hicho kilikwama kupanda baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-1.
Mechi ya mwisho leo itapigwa kwenye Uwanja wa Kituo cha TFF Kigamboni jijini Dar es Salaam, ambapo wenyeji maafande wa Transit Camp iliyoifunga TMA ugenini Arusha bao 1-0, itaikaribisha Bigman iliyotoka sare ya bao 1-1 na Polisi Tanzania.
Kocha wa Polisi Tanzania, Mbwana Makata alisema katika mechi iliyopita na Bigman walistahili kushinda ingawa miongoni mwa mambo yanayowaangusha ni kukosa umakini hususan katika dakika za mwishoni, jambo analopambana kulifanyia kazi siku baada ya siku.
“Baada ya kuongoza bao 1-0, wachezaji waliona kama mechi imeisha kwa sababu walishindwa kumuheshimu mpinzani na mwisho wakasawazisha na kuisha 1-1, tunapaswa kuondokana na hali hiyo kutokana na ushindani huu unaoendelea,” alisema Makata.