Dodoma. Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko, ametoa onyo kwa wadau na taasisi zote zinazohusika na usimamizi wa kemikali hatarishi ya ‘ammonium nitrate’ kuhakikisha umakini unaongezwa katika utunzaji na usafirishaji wake, ili kuepusha madhara kwa jamii.
‘Ammonium nitrate’ ni kemikali inayozalishwa viwandani, na hutumika kama chanzo cha nitrojeni katika mbolea.
Hata hivyo, kemikali hiyo pia hutumika kutengeneza vilipuzi vinavyotumika kwenye shughuli za uchimbaji migodi.
Dk Mafumiko amesema kuwa kutotunza kemikali hiyo ipasavyo huongeza hatari ya madhara makubwa, kwani wahalifu wanaweza kuitumia kama chanzo cha milipuko mikubwa, na hivyo kusababisha maafa kwa binadamu pamoja na uharibifu wa mali.
Akizungumza leo Novemba 22,2025 kwenye kikao kazi cha Taasisi za Udhibiti na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kilichofanyika katika Ukumbi wa Dk Manyele jijini Dodoma, Dk Mafumiko amesema pamoja na kemikali hiyo kuwa muhimu kwa sekta mbalimbali, inahitaji udhibiti wa karibu na wa kitaalamu.
“Tulikutana kipindi cha nyuma na tukajadili namna bora zaidi ya kusimamia kemikali, hususan ‘Ammonium Nitrate’, ni kweli ina faida kubwa katika nyanja mbalimbali, lakini bado inahitaji usimamizi makini na wa karibu,” amesema Dk Mafumiko.
Dk Mafumiko amesema ushirikiano miongoni mwa taasisi zote zinazojishughulisha na kemikali hizo ni muhimu ili kuhakikisha usalama wakati wa kusafirisha na wakati wa kuhifadni kwenye maghala.
Aidha, amewashukuru wadau wote kwa kujitokeza licha ya majukumu yao mengi, akibainisha kuwa kikao hicho ni hatua muhimu katika kujadili mustakabali wa usimamizi salama wa kemikali hatarishi nchini.
“Nawashukuru kwa kuitikia wito wa kikao hiki muhimu najua mmejitolea muda wenu, na kwa niaba ya Menejimenti pamoja na Bodi ya Wakurugenzi, nawapongeza sana,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti GCLA, Daniel Ndiyo, amewakumbusha wasimamizi hao wa usalama kuwa matumizi ya ‘Ammonium Nitrate’ ni makubwa kwenye migodi na shughuli za ulipuaji.
Amezitaka taasisi kama Tume ya Madini, Mamlaka ya Mbolea, na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuimarisha usimamizi kulingana na majukumu yao ili kuzuia matumizi mabaya au uvurugaji wa taratibu za kiusalama.
Ikumbukwe kwamba Sheria ya kemikali za Viwandani na Majumbani Na.3 ya Mwaka 2003 inaelekeza GCLA kufanya ukaguzi wa maeneo yote yanayohusika na shughuli za kemikali ikiwamo maghala, bandari, viwanja vya ndege na mipaka.
Pia, kutoa elimu kwa umma kuhusiana na huduma zitolewazo na mamlaka mfano matumizi salama ya kemikali ili kulinda afya ya binadamu na mazingira.