Nahodha Mtibwa atuma salamu KMC

NAHODHA wa Mtibwa Sugar, Oscar Masai amezitaja dakika 90 bora dhidi ya KMC katika mchezo utakaopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, lakini akielezea hofu yao kwa timu ambayo imejerehiwa.

Mtibwa Sugar ambayo itakuwa mwenyeji wa mchezo huo inatarajiwa kutua leo jijini humo kujiwinda dhidi ya KMC ambayo juzi ilipoteza mchezo wa sita wa Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kuchapwa na JKT Tanzania kwa bao 1-0.

Akizungumza na Mwanaspoti, Masai alisema na wanatua wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza kwenye uwanja huo dhidi ya Yanga kwa mabao 2-0, lakini wapo tayari kwa ushindani kutokana na maandalizi waliyoyafanya.

“Tunaingia kucheza mchezo huo tukiwa chini ya kocha mpya ambaye amekuja na mbinu mpya na ameona upungufu na kuufanyia kazi kabla ya kuvaana na wapinzani wetu. Matarajio ni kukusanya pointi tatu muhimu na kujiweka kwenye mazingira mazuri ya ushindani,” alisema nahodha wa kikosi hicho ambacho kipo chini ya kocha Yusuf Chipo.

“Mpinzani wetu tutaingia kwa kumheshimu licha ya kutokuwa na matokeo mazuri kwenye mechi zaidi ya tatu mfululizo, inawezekana akaibukia kwetu na sisi hatutarajii hilo kwani tunatambua umuhimu wa mchezo huo ambao endapo tutapata matokeo mazuri tutarudi kwenye morali.”

Masai alisema ujio wa Chipo umeongeza morali na ushindani kikosini kutokana na kila mchezaji kutaka namba katika kikosi cha kwanza, hivyo anaamini hiyo inaweza kuwa chachu ya ubora na kutoa ushindani kwa mpinzani wao.

“Kama kila mchezaji anataka kuonyesha kuanzia uwanja wa mazoezi hii inaweza kuwa chachu ya ushindani na tunaweza kufanya vizuri hadi kwenye mchezo wetu dhidi ya KMC ili kujihakikishia nafasi ya kucheza chini ya Chipo.”