Pedro katika mtihani wa rekodi ya Yanga na Waarabu CAF

KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, leo Jumamosi Novemba 22, 2025, ana mtihani mgumu kikosini hapo katika michuano ya kimataifa atakapoikabili AS FAR Rabat kutoka Morocco.

Pedro raia wa Ureno, aanza kimataifa baada ya kuiongoza Yanga mechi mbili za Ligi Kuu Bara na kushinda zote dhidi ya Mtibwa Sugar (2-0) na KMC (4-1).

Wakati leo Yanga ikiwa mwenyeji wa AS FAR Rabat kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, rekodi zinawanyima furaha mbele ya Waarabu.

Mechi hiyo ya kwanza hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, imepangwa kuanza saa 10:00 jioni.

Rekodi zinaonyesha, Yanga hii ni mara ya sita inacheza hatua ya makundi michuano ya CAF ndani ya kipindi cha miaka kumi kuanzia 2016, na zote hizo inaanza na timu zenye asili ya Waarabu.

Katika mechi tano zilizopita dhidi ya Waarabu, Yanga imepoteza zote, hali inayomfanya Pedro leo kuingia uwanjani na mtihani wa kuvunja rekodi hiyo mbovu kwa kikosi hicho.

Si kupoteza tu, bali Yanga mechi hizo haijafanikiwa kufunga bao lolote ukiwa ni mtihani mwingine kwa Pedro, kwanza kufunga bao, pili kutopoteza mbele ya Waarabu kwenye mechi ya kwanza ya kundi michuano ya CAF.

Ilianza Juni 19, 2016 ambapo Yanga ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika, mechi ya kwanza ya kundi ilianza na MO Bejaia ya Algeria, ikapoteza kwa bao 1-0.

Mei 6, 2018, Yanga ilishiriki Kombe la Shirikisho na hatua ya makundi ilianza dhidi ya USM Alger kutoka Algeria, ikapoteza kwa mabao 4-0.

Msimu wa 2022-2023, Yanga ilianzia Ligi ya Mabingwa, lakini ikaangukia Shirikisho baada ya kutolewa na Al Hilal hatua ya pili, ikakutana na Club Africain, ikaitoa kwa jumla ya bao 1-0 na kufuzu makundi.

Hatua ya makundi, mechi ya kwanza ilikutana na US Monastir ya Tunisia na kupoteza kwa mabao 2-0.

Msimu wa 2023-2024, ilikuwa Ligi ya Mabingwa, mechi ya kwanza makundi ilikutana na Al Hilal ya Sudan na kufungwa 2-0, kisha 2024-2025, ilifungwa 3-0 na CR Belouizdad ya Algeria, ikiwa mechi ya kwanza hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa.

“Tuna kikosi cha wachezaji 32. Kwa bahati mbaya, wawili ni majeruhi. Hata hivyo, bado tuna faraja na motisha ya kufanya kazi kwa bidii kwa sababu tuna lengo kubwa mbele yetu. Ni changamoto kubwa, lakini tupo tayari kupambana na kushinda,” amesema Pedro.

Yanga katika kundi B mbali na AS FAR Rabat ya Morocco, imepangwa pia na Al Ahly ya Misri na JS Kabylie kutoka Algeria.

Baada ya mechi ya leo, wikiendi ijayo ya Novemba 28, 2025 itakuwa Algeria kukabiliana na JS Kabylie, kisha itasubiri hadi Januari kupambana na Al Ahly nje ndani.

Katika kundi hilo, AS FAR Rabat imebeba kombe moja la Ligi ya Mabingwa, JS Kabylie imeshashinda mataji hayo mawili, huku Al Ahly ikiwa bingwa wa kihistoria ikishinda 12. Yanga bado.