Dar es Salaam. Eneo la Tabata Segerea, jijini Dar es Salaam, Samwel Petro (26), anayefahamika kwa jina la biashara Masheyn Perfume, ndiko anakojipatia kipato cha siku cha kuendesha maisha yake.
Ni wa kawaida lakini safari yake si ya kuichukulia powa kwa kauli ya watoto wa mjini. Petro ni wa kupigiwa mfano kwa namna ambavyo mitandao ya kijamii ikitumiwa kwa ubunifu inaweza kubadili kabisa maisha ya kijana.
Hakufika mbali kielimu, alihitimu tu elimu ya msingi lakini hiyo haikumzuia kusaka maisha. Alianza kuuza manukato ya kupima, biashara ambayo leo imekuwa uti wake wa mgongo.
Kupitia mtandao wa kijamii wa Tiktok, amejitangaza na kujizolea wateja wa aina mbalimbali. Unaweza kusema amejizolea umaarufu zaidi kutokana na kipimo chake cha kipekee, manukato ya Sh500 ‘jero’ kwa matumizi ya siku moja.
Unapohitaji huduma unakwenda, unapewa manukato kwenye nguo ulizovaa, unanukia siku nzima na maisha yanaendelea.
Katika mahojiano na Mwananchi hivi karibuni anasema, biashara hiyo anayoifanya kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa imemwezesha kuendesha maisha yake ya kila siku na hatamani kuajiriwa zaidi ya kujiajiri.
Kwa mujibu wa Petro, wazo la biashara hiyo halikuzaliwa kirahisi, awali aliiona fursa ya kuwapo uhitaji wa vijana kuonekana nadhifu na kunukia kwa gharama nafuu.
Alipoanza kuuza kipimo cha Sh3,000 kwenye chupa ndogo aligundua kundi kubwa la vijana halikumudu. Wengine walimwomba awapulizie tu japo kidogo ili waendelee kunukia siku hiyo.
Petro akaona hapo ndipo fursa ilipo. Akaanzisha kipimo cha Sh500 na mambo yakabadilika.
“Wengine walikuwa wanakuja kuomba niwapulizie japo kidogo ili wanukie kwa siku hiyo kwa kuwa hawana fedha za kununua manukato, hata hiyo Sh3,000,” anasema na kuongeza:
“Nilikuwa nikiwasaidia lakini baadaye nikaona fursa, naweza kuwawekea kipimo cha Sh500 na mtu akanukia.”
Anaeleza mtu anapotaka kuuziwa manukato kwa kipimo cha Sh500 anaruhusiwa kuchagua aina moja pekee.
Kabla ya ubunifu huo, anasema alikuwa akipata kati ya Sh20,000 na Sh50,000 kwa siku. Sasa anakusanya kati ya Sh30,000 hadi Sh70,000 au zaidi kwa siku nyingine.
“Ubunifu huu umenisaidia kupata wateja wa aina mbalimbali hata wale wenye kipato cha chini,” anasema.
Hata hivyo, anasema katika biashara siku hazifanani akieleza: “Kuna siku wateja wanakuwa wengi na zingine wanakuwa wachache. Lakini nashukuru sikosi chochote kitu kwa ajili ya kuitunza familia.”
Safari yake ya kufika alipo imetawaliwa na milima na mabonde.
Baada ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2014 mkoani Manyara, alivunjwa moyo na hali ngumu ya kiuchumi ya familia yake iliyosababisha ashindwe kuendelea na masomo.
Anasema katikati ya ugumu huo wa maisha akaamua kuianza safari ya kusaka maisha Dar es Salaam.
Akiwa ndani ya jiji, ili mkono uende kinywani anasema alianza kazi ya kuosha magari na hata kuuza genge.
Hatua kwa hatua akaanza kubadilisha kazi akilenga kusanya mtaji lengo likiwa kufanya biashara ya manukato.
Kujituma inalipa. Anasema jitihada zake zilimwezesha kupata mkopo wa Sh300,000 kutoka kwa anayemwita msamaria mwema alizozitumia kuanzisha biashara ya manukato.
Hapo ukawa mwanzo wa safari yake ya mafanikio, akieleza hakukaa na deni, alimudu kurejesha mkopo na papo hapo kuendelea na biashara.
Anasema mitandao ya kijamii imekuwa nguzo yake muhimu akieleza bila Tiktok, pengine wateja alionao leo asingewafikia.
Kwangu mitandao ya jamii si sehemu ya kuburudika pekee, bali ni jukwaa la kujijenga. Ni sababu ya kuonekana, kupata wateja na kuongeza kipato.
“Huwa natafakari bila mitandao ya kijamii kuwapo pengine nisingekuwa na wateja kama nilionao sasa. Mitandao hasa Tiktok imenifanya kujulikana na watu wengi na hata kukuza biashara yangu,” anasema na kuongeza:
“Kuna watu wanaodhani mitandao ni kwa ajili ya kujiburudisha tu, hapana. Mimi ni mfano kwamba, kama ukitumia kwa umakini, nidhamu na ubunifu, inaweza kukuwezesha kupata kipato.”
Anawashauri vijana wenzake kutokata tamaa, akisema kila mmoja ana lake analolipitia lakini wazo moja, jitihada na nidhamu vinaweza kubadili maisha.
Petro anasema bado ana ndoto, anataka kukuza biashara yake, kupata wateja zaidi na kurudi shule ili amalize elimu ya sekondari na kukwea ngazi hadi chuo kikuu.
Mbali ya hayo, anasema anataka kukuza kipaji chake cha muziki na hasa wa nyimbo za dini maarufu Injili.
Wateja wake nao wana maneno yao. Miongoni mwa hao ni Ashura Hassan, mkazi wa Tabata Segerea.
Anasema huduma ya manukato ya kupima inamuokoa siku ambazo hana fedha ya kununua chupa nzima kwani anachofanya ni kutembea tu kuelekea kwa Petro, anapuliziwa na maisha yanaendelea.
“Hata siku nikiwa sina pesa na nimeishiwa manukato nakuja ananipulizia naendelea kunukia,” anasema.
John Makongoro yeye anasema hapendi kupoteza fedha za kununua manukato mengi, wakati anachohitaji ni kunukia kwa siku moja pekee na kwa Petro hilo ni rahisi.
“Siyo lazima ninunue nyingi nikapoteza pesa. Pale ninapohitaji ninafika hapa anaipulizia ninanukia siku nzima,” anasema.