Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linamshikilia Mwalimu wa Shule ya Awali ya ‘Saint Clemence’, Clemence Mwandambo mkazi wa Uzunguni A jijini humo kwa tuhuma za uchochezi.
Mwandambo ambaye amekuwa maarufu mitandaoni kwa maneno yake ikiwano maarufu la ‘Nachoka baba yenu Clemence Mwandambo’ inaelezwa alikamatwa na Jeshi la Polisi jana Novemba 21.
Mwandambo ambaye ni mkazi wa jijini Mbeya kupitia mitandao ya kijamii haswa Facebook na Instagram amejizolea umaarufu kutokana na video zake anazochapisha mitandaoni.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga iliyotolewa leo Jumamosi Novemba 22, 2025 imethibitisha jeshi hilo kumshikilia msanii huyo kwa tuhuma za uchochezi.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa jana Ijumaa Novemba 21, 2025 saa 5:20 asubuhi maeneo ya Uzunguni jijini humo kwa madai ya kutoa na kusambaza maneno ya uchochezi na uchonganishi kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii.
“Mtuhumiwa alikamatwa akitoa na kusambaza maneno ya uchochezi na uchonganishi kupitia akaunti zake za Facebook na Instagram, upelelezi unakamilishwa ili hatua nyingine za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake,” imeeleza taarifa ya Kamanda Kuzaga.