TIMU ya Taifa ya wanawake ya Futsal inaanza karata yake ya kwanza kesho kusaka taji la Kombe la Dunia la futsal dhidi ya Ureno mechi itakayopigwa saa 8:30 mchana katika Uwanja wa PhilSports Arena, Pasig nchini Ufilipino.
Mashindano ya futsal yanafanyika nchini Ufilipino yalianza Novemba 21 na fainali itapigwa Desemba 7 yakijumuisha timu 16, huku Tanzania ikipangwa kundi C na timu za Ureno, Japan na New Zealand.
Kundi A lina wenyeji Ufilipino, Poland, Morocco na Argentina ilgali kundi B likiwa na Hispania, Thailand, Colombia na Canada, huku lile la D lina mabingwa wa zamani Brazil, Iran, Italia na Panama.
Kocha mkuu wa Tanzania, Curtis Reid amesema wana mechi ngumu dhidi ya Ureno na benchi lao la ufundi limepambana kuhakikisha linaondoa presha kwa wachezaji ili waweze kufanya vizuri.
“Kila kitu kinaonekana kuwa sawa. Tuko tayari kwa ajili ya mechi na tumewaandaa vizuri mabinti na kuwaondolea presha wawe tayari kwa ajili ya mechi hiyo ngumu,” amesema Reid.
Baada ya mechi hiyo ratiba inaonyesha Tanzania itashuka tena uwanjani Novemba 26 dhidi ya New Zealand na kumaliza makundi Novemba 29 itakapokipiga na Japan, mechi zote zikipigwa Philsports Arena Pasig.
Tanzania na Morocco ndizo timu pekee kutoka Afrika zilizofuzu mashindano hayo, ikiwa mara ya kwanza kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuyaanzisha, lakini kwa duniani hii ni mara ya pili baada ya kufanyika 2010 nchini Hispania ambako Brazil ilitwaa ubingwa.
Tanzania ilifuzu baada ya kufika fainali CAF ambako ilipoteza dhidi ya Morocco kwa mabao 4-3, hivyo bingwa na mshindi wa pili kufuzu moja kwa moja.
Fainali za Mataifa ya Afrika za Futsal ambazo zilitumika kupata timu hizo mbili zilifanyika Morocco kuanzia Aprili 22 hadi Aprili 30, 2025.
Kwa Afrika hii ilikuwa mara ya kwanza futsal kuandaliwa na CAF upande wa wanawake. Mataifa tisa yalishiriki.
Katika Bara la Ulaya, UEFA ilizindua mashindano ya kwanza ya futsal kwa wanawake Februari 2019 yakihusisha timu kutoka mataifa ya Hispania, Ureno, Urusi na Ukraine.