……………..
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa siku saba kwa Wakandarasi Wazawa wanaotekeleza miradi ya dharura katika barabara ya Gairo – Dodoma – Kintinku kukamilisha kuweka tabaka la juu la lami katika maeneo yanayokarabatiwa ili kuruhusu magari kupita juu ya barabara na kuondokana na adha ya foleni katika barabara za mchepuo.
Ulega ametoa maelekezo hayo leo Novemba 22, 2025 Mkoani Dodoma wakati akikagua utekelezaji wa miradi hiyo inayoendelea na ile iliyokamilika katika eneo la Mbande, Mtanana, Pandambili na Silwa Mkoani humo na kuridhishwa kwa hatua mbalimbali zilizofikiwa katika maeneo yote.
Ulega amewataka Wakandarasi hao kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana na kukamilisha kwa wakati na ubora unaotakiwa na kuelekeza uongozi wa Wilaya ya Kongwa kuendelea kuimarisha ulinzi wakati wote wa utekelezaji wa mradi.
“Nimekagua na nimeona athari za mvua zinazonyesha kutoka mikoa jirani ya Manyara, Ninatoa wiki moja kwa Wakandarasi kukamilisha kazi hiyo ili mvua hizi zinapoanza kunyesha Mkoani Dodoma isikute wananchi bado wapo kwenye barabara ya mchepuo”, ameeleza Waziri Ulega.
Aidha, Ulega ameelekeza Wakandarasi hao kuhakikisha wanaendelea kukamilisha kazi zingine zilizobakia ikiwemo za ufungaji wa taa za barabarani 300 pamoja na kuweka alama za barabarani wakati magari yakiendelea kupita katika barabara hiyo.
Wakandarasi hao ni Kings Builder Company anayetekeleza ujenzi wa makalvati makubwa katika eneo la Mbande na Mkandarasi Technics Construction group anayetekeleza ujenzi wa makalvati eneo la Pandambili na Silwa katika barabara hiyo.
Kadhalika, Ulega amewataka wakandarasi wazawa kutekeleza kazi zao vizuri kwa kuwa ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Wizara kutoa kipaumbele kwa Wakandarasi wazawa wenye uwezo, utayari na ubora wa kazi zao.
“Tunayo maelekezo ya kuwapeni kazi nyingi za ujenzi lakini hatuwezi kuwapa tu kama hamfanyi kazi nzuri, Jitahidini kufanya kazi nzuri kwa wakati na ubora”, amesisitiza Ulega.
Ulega amekagua na kuridhishwa na ujenzi wa makalvati makubwa na unyanyuaji wa tuta la barabara eneo la Mtanana ambalo limetekelezwa na Mkandarasi Estim Construction kwa gharama ya Shilingi Bilioni 26 na kuahidi kulifanyia kazi suala la kuongezewa upana wa barabara kwa ajili ya wananchi kufanya biashara.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Dodoma Eng. Zuhura Amani ameeleza utekelezaji wa ujenzi wa makalvati na unyanyuaji wa tuta la barabara katika eneo la Mbande umefikia asilimia 88 na unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 7.9.
Halidhalika, Eng. Zuhura ameeleza kuwa asilimia 95.4 zimefikiwa katika utekelezaji wa mradi wa makalvati makubwa na unyanyuaji wa tuta la barabara eneo la Pandambili na Silwa na mradi unagharimu Shilingi Bilioni 2.8.