Utoro, mimba vyaongoza mdondoko wa wanafunzi

Dar es Salaam. Mimba na utoro vimeendelea kuwa sababu kuu za wanafunzi kuacha shule katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania kwa mwaka 2024, kama inavyoelezwa katika ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Ripoti ya Statistical Abstract ya mwaka 2024 iliyochapishwa Septemba 30, 2025 katika tovuti ya NBS inaonyesha kuwa utoro ulibeba asilimia 99.21 ya wanafunzi wote walioacha shule za msingi mwaka 2024 na asilimia 97.12 kwa upande wa sekondari.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanafunzi 157,350 kati ya 158,594 walikatisha masomo ya elimu msingi mwaka 2024 sababu ikiwa utoro uliokithiri.

Takwimu hizo zinafanya sababu nyingine kama vifo, utovu wa nidhamu na mimba zilizotajwa katika ripoti kuwa na idadi chini ya asilimia moja.

Uchambuzi unaonyesha wanafunzi 993 walifariki dunia, utovu wa nidhamu walikuwa wanafunzi 68, huku mimba zikiwaondoa shuleni wanafunzi 183 katika elimu ya msingi.

Hali hiyo ni tofauti kwa upande wa shule za sekondari kwani mbali na utoro uliobeba asilimia 97.12, mimba zilichangia asilimia 1.57 ya walioacha shule.

Kati ya wanafunzi 148,337 wa sekondari walioacha shule katika kipindi husika, 144,076 ilikuwa ni kwa utoro, 2,330 wakiacha kwa sababu ya kupata mimba, utovu wa nidhamu 1,418 na waliofariki dunia ni 513.

Inaonyeshwa katika ripoti kuwa, wanafunzi wengi wanatoka mikoa ya Mwanza, Geita, Tabora, Dodoma na Kagera katika ngazi zote za elimu ya msingi na sekondari.

Akizungumzia suala hili, mdau wa elimu, Nicodemus Shauri, ametaka kufanyike tafiti za kina ili kutokomeza tatizo la wanafunzi kukatisha masomo.

Amesema moja ya sababu ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kuongoza kwa watoto wengi kuacha shule ni shughuli za kiuchumi zinazozunguka eneo hilo, ambazo huwavutia kuacha masomo kwa sababu ya kuwa na uwezo wa kushika fedha mapema.

Baadhi ya watu katika ukanda huo hujishughulisha na uvuvi, biashara, kilimo, ufugaji na uchimbaji migodini.

“Fursa ya kupata hela inawafanya vijana wengi hasa wa kiume ambao hawana uwezo mzuri kitaaluma, kuingia katika shughuli hizo. Wengine hawana mahitaji muhimu ya shule kutokana na familia zao kuwa maskini,” amesema.

Vilevile, uwepo wa njia za usafirishaji kwenda nchi jirani unatajwa na Shauri kama moja ya sababu ya wasichana wengi kupata mimba.

Shauri anazungumzia umuhimu wa elimu akitaka liangaliwe zaidi ili kutambua kuwa wakazi wa eneo hilo wana ufahamu kwa kiasi gani.

Anasisitiza matumizi ya elimu ya amali kama njia ya kuwavuta watu kwenda shule kujifunza ufundi.

“Siku hizi shule hazivutii, hakuna hata viwanja vya michezo, hii imefanya wengi kubaki nyumbani. Wengine wanaweza kuwa hawapendi shule, lakini michezo inawavutia kwa sababu wanajua labda mpira. Pia kukosekana kwa chakula ni jambo lingine linalowafanya wanafunzi kushindwa kukaa shuleni,” amesema.

Kukosekana kwa walimu wa kutosha ni sababu nyingine, akisema baadhi ya wanafunzi wakiwa hawaelewi kinachofundishwa wanaona bora kuacha shule wafanye mambo mengine.

Ameshauri kuwapo vivutio mbalimbali, ikiwemo michezo, mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia ili wanafunzi wakae shuleni.

Ochola Wayoga, mdau wa elimu aliyewahi kuwa Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet), amesema ni vyema wanaoacha shule kwa ajili ya utoro wawekwe kwenye makundi ili iwe rahisi kushughulika nao kutokana na sababu zao.

Amesema hilo ni kwa sababu hadi mtoto anaacha shule, huwa zinafanyika jitihada mbalimbali, ikiwemo ufuatiliaji kwa wazazi au walezi kuitwa na wanafunzi kutafutwa kwa njia mbalimbali.

“Wanaoacha shule wengi huwa wanaolewa au kuoa, kwenda kwenye shughuli za kilimo au familia zao, hususani za jamii za wafugaji kuhamia mbali na shule, sehemu ambazo ni mbali kuwafuatilia,” amesema.

Amesema kukosekana kwa miundombinu rafiki ya kujifunzia kama madarasa ya kutosha yenye madawati, vyoo, walimu wa kutosha ni sababu zinazofanya wanafunzi kusalia nyumbani kutokana na kutovutiwa.

“Hatujafanya kiasi cha kutosha katika kuainisha vipaumbele vyetu katika sekta ya elimu. Kitu kama chakula, Serikali ikiamua inaweza kutoa kwa wanafunzi wote wa shule ya msingi hadi sekondari kwa sababu fedha zipo,” amesema.

Ili kukabiliana na tatizo la wanafunzi kuacha masomo, ameshauri wazazi kuwajibishwa moja kwa moja kwa kuchukuliwa hatua ili wawe watu wa kwanza kuhakikisha watoto wanapoanza shule wanamaliza, badala ya wao kuwa wasababishaji.

“Ingekuwa kila mzazi ambaye mtoto wake ataacha shule anafungwa jela miezi mitatu, hakuna ambaye angekaa kusubiri kifungo badala yake angekuwa akipambana kuhakikisha mwanaye anamaliza shule na akionyesha kusuasua angekuwa akiomba msaada huku na kule ili awe salama,” amesema.

Alipozungumza na Mwananchi, Novemba 16, 2025, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Caroline Nombo alisema wako katika hatua za kuandaa mfumo mzuri wa kukusanya takwimu ili kuondoa mkanganyiko uliopo wa wanafunzi kuandikishwa shule lakini hawamalizi.

Mfumo huo alisema pia utasaidia kufanya ufuatiliaji wa mwanafunzi tangu anapoanza darasa la awali shule yoyote iwe ya Kiingereza, kimataifa au Serikali ili kuweka urahisi wa kujua wanafunzi wako wapi na wanafanya nini.

“Sitaki kuamini kuna mdondoko kwa kiasi, tunatakiwa kuthibitisha hizi takwimu. Lakini kupitia mfumo huu tutaweza kujua kwani tunatambua kuna wengine wanakariri wengine wanahama nchini lazima tuzithibitishe, hata akienda mfumo wowote lazima tujue,” alisema.

Profesa Nombo alisema hayo alipojibu swali la mwandishi wa Mwananchi kuhusu zaidi ya wanafunzi 300,000 walioacha masomo njiani ambao walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022 lakini hawakufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu.

Alisema ujio wa jamii namba ambayo itakuwa ikisajili hadi watoto tangu wanazaliwa pia itakuwa na mchango chanya katika kurahisisha ufuatiliaji wa wanafunzi tangu wanaandikishwa shule ili kujua wanatoka wapi wanakwenda wapi.

“Lakini hata wanaodondoka, Serikali imeweka nafasi ya wao kurudi tena shuleni na wapo wengi waliorudi katika mfumo usio ramsi na wengine wamerudi katika mfumo rasmi, wengi wamerudi na wengine wameenda hata vyuo,” alisema.

Vilevile, alisema Serikali inasaidiana na jamii ili kuhakikisha watoto wanaandikishwa shule, kufuatilia maendeo yao kwa kuhakikisha vijana wanaokwenda wanabaki shule, huku wakitengenezewa mazingira mazuri.

“Sisi kama Serikali tunapunguza umbali wa wanafunzi kwenda shule kupitia ujenzi wa shule katika maeneo wanayoishi, kwani ilikuwa moja ya sababu na hii imekuwa na faida kwani watoto wanakwenda shule na kurudi kirahisi sambamba na kujenga mabweni,” alisema.