VIONGOZI ARDHI SACCOS WATAKIWA KUWA WABUNIFU

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Lucy Kabyemera amewataka viongozi wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi (Ardhi Saccos Ltd) kubuni mbinu za kujitangaza pamoja na kujitanua nje ya wizara ili kuwa na idadi kubwa ya wanachama watakaokiwezesha chama hicho kuongeza mtaji.

Aidha, ameutaka uongozi huo kubuni miradi mbalimbali ikiwemo viwanja katika maeneo yasiyo na migogoro ili kuwanufaisha wanachama sambamba na kuongeza mtaji kwa kuuza viwanja.

Bi. Kabyemera ametoa wito huo leo tarehe 21 Novemba 2025 wakati wa kufungua mkutano wa tano wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi (Ardhi Saccos) uliofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Ardhi katika mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

‘’Mmeanza kubuni miradi mbalimbali ya kuwaongezea kipato naomba mharakishe na muongeze jitihada za kutanua wigo kwa kutafuta maeneo yasiyo na migogoro ili yauzike’’ amesema.

‘’Niwapongeze kwa usimamizi mzuri wa Saccos na kila mmoja wenu awe na wajibu kuhamasisha wanachama kujiunga ili tuwe na wanachama wengi zaidi’’ amesema Lucy

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ardhi Saccos Ltd Bw. Preygod Shayo amesema, Ardhi Saccos Ltd inazidi kukua na wao kama uongozi wanafanya jitihada kubwa kuhakikisha wanakuwa na wanachama wengi zaidi.

‘’Chama kinazidi kukua na tunafanya jitihada kubwa ili wanachama wajiunge na ni matarajio yetu kufikia Januari tutakuwa na miradi ya kuongeza kipato nje ya akiba na mikopo’’ amesema.

Kwa sasa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi (Ardhi Saccos Ltd) Kina takriban wanachama 300 kutoka Makao Makuu ya Wizara, Ofisi za Ardhi za Mikao pamoja na halmashauri.