Wakulima watia shaka utolewaji fedha kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi

Dar es Salaam. Wakati dunia inaangazia kwa makini majadiliano ya Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaofanyika Belem, nchini Brazil, wakulima wadogo wa Afrika Mashariki na hasa wale wa vijijini nchini Tanzania, wanaendelea kubeba mashaka kuhusu mustakabali wao.

Rais wa Shirikisho la Wakulima wa Afrika Mashariki (EAFF), Elizabeth Nsimadala, amsema licha ya matumaini waliyoyabeba kuelekea mkutano huo, bado hawaamini kama fedha za Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu zitawafikia moja kwa moja.

Akizungumza kuhusu ufadhili wa Dola 250 milioni za Marekani (takribani Sh600 bilioni) uliopitishwa kwa mwaka 2026, Nsimadala amesema kiwango hicho ni kidogo mno kulinganisha na ukubwa wa madhara ambayo wakulima wamekuwa wakipitia kila msimu. 

“Tunatarajia kunufaika, lakini hatuweki matumaini. Kiwango kilichotengwa ni kidogo ukilinganisha na mahitaji. Ushindani utakuwa mkubwa, mbaya zaidi mifumo iliyopo ya upatikanaji wa fedha haikuwahi kuelekezwa kwa vikundi vya wakulima moja kwa moja,” anasema.

Nsimadala ambaye amehudhuria mkutano huo anasema fedha nyingi huishia kupitia serikali za kitaifa, benki za kimataifa au mifuko mikubwa ya kimataifa, hivyo mara nyingi haziwafikii wakulima.

Anaeleza kuwa utafiti wa Family Farmers for Climate Action unaonyesha kati ya Dola 2.6 bilioni (Sh6.302 trilioni) zilizowekezwa na GEF na GCF kati ya 2019 na 2022, ni theluthi moja pekee ilielekezwa kwenye miradi ya kilimo endelevu inayowagusa wakulima wadogo.

Anasema hakuna hata senti iliyokwenda moja kwa moja kwenye mashirika ya wakulima.

“Utafiti wa IPCC na OECD unaonyesha wazi kuwa fedha zinapofikishwa moja kwa moja kwa walengwa ndiko kunakoleta matokeo makubwa. Sisi EAFF tumeliona hili kwa macho yetu,” amesema Elizabeth ambaye ni mkulima kutoka Uganda.

Amesema walishirikiana na Serikali ya Djibouti baada ya ukame ulioangamiza mifugo, wakaleta mbegu za mbuzi wa maziwa wanaostahimili ukame kwa uwekezaji wa Dola 75,000 (Sh187.5 milioni), ambao baadaye uliongezeka hadi zaidi ya Dola 500,000 (Sh1.25 bilioni) na kuwafikia wakulima zaidi ya 500.

“Haya ni mfano kuwa fedha zikifika moja kwa moja kwa wakulima zinabadili maisha,” amesema.

Akieleza kuchoshwa na ahadi zisizotekelezwa, Elizabeth anasema: “Tumechoka na hotuba zisizokuwa na matokeo. Tunataka ufadhili wa moja kwa moja, unaoweza kuwafikia wakulima wanaopambana na ukame, mafuriko, uharibifu wa udongo na mavuno kushuka.”

Anayoyazungumza Elizabeth yanaendana na wanayopitia wakulima wa Shinyanga na Mwanza, nchini Tanzania.

Kwiyolecha Nkilijiwa, mkulima wa dengu kutoka Kata ya Salawe, wilayani Shinyanga, anasema wanahitaji msaada wa haraka na wa moja kwa moja, si ahadi zinazosubiriwa kwa miaka.

“Sisi tunataka mikakati ya kurejesha uoto wa asili ili mvua irejee, tupate visima virefu na mabwawa ya kutusaidia kupata maji, bila hivyo hata tukipewa fedha hazitatusaidia,” anasema.

Si yeye pekee anayehofia athari za mabadiliko ya tabianchi, huku kukiwa na sintofahamu ya kupata fedha hizo.

Kulwa Charles, mkulima wa mpunga kutoka Kijiji cha Isela, wilayani Kwimba, anasema kilimo kwenye maeneo yao kimefikia mahali pa kutisha.

“Matumizi ya dawa yamechosha ardhi, mvua hazitabiriki. Kila mwaka uzalishaji unashuka. Ndiyo maana tunasubiri kuona COP30 itatoa suluhisho gani, lakini hatuna uhakika kama fedha zitatusaidia sisi wakulima wadogo vijijini,” anasema.

Wakulima hawa wanatoa ushuhuda unaoonyesha jinsi hali ilivyo mbaya zaidi ndani ya miaka mitano.

Nkilijiwa, ambaye zamani alivuna gunia nane hadi 10 za dengu kwa ekari, sasa anapata saba hadi nane. Mbali ya hayo, aliamua kupunguza ukubwa wa shamba kutoka ekari 10 hadi mbili kutokana na hasara na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji.

Kuhusu mpunga, Kulwa anasema mavuno yameshuka kutoka gunia 60 hadi 65 kwa ekari hadi 50–60, huku akilazimika kupunguza ukubwa wa shamba kutokana na gharama zisizohimilika.

Kwa upande wake, Charles Ndugulile wa Kata ya Mwamala, wilayani Kwimba mkoani Mwanza, anasisitiza umuhimu wa mbegu zinazostahimili ukame na elimu.

“Elimu kwa wakulima ni muhimu, lakini tunahitaji mbegu ambazo zinaweza kuvumilia hali mbaya ya hewa. Bila hivyo, mazao yanaendelea kushuka,” anasema.

Ndugulile anasema uzalishaji wa mpunga umeshuka hadi magunia 30 hadi 40 kutokana na ukosefu wa mvua na kutotabirika kwa msimu.

Anasema elimu ya kilimo imepunguza kasi ya hasara kwa kiasi fulani, lakini bado wanategemea mvua.

Katika alizeti, anasema ameongeza uzalishaji baada ya kupata mbinu bora lakini bado hana hakika kama fedha za kimataifa zitawafikia ili kuongeza uzalishaji zaidi.

Kwa Antony Ngeleja, mkazi wa Shilabela, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, upandaji miti na matumizi ya majiko ya gesi ni hatua muhimu kwao, lakini bila rasilimali kuwafikia moja kwa moja, juhudi hizi zitabaki historia.

“Tunahamasishwa kutunza mazingira, kupanda miti, kutumia gesi lakini bila msaada thabiti hatuwezi kupiga hatua,” anasema.

Serikali ya Tanzania kupitia AGN imetangaza kuwa inaweza kupata hadi Dola 20 milioni (Sh50 bilioni) kutoka Mfuko wa Hasara na Uharibifu baada ya kutengwa kwa Dola 250 milioni kwa mwaka 2026.

Mshauri wa Rais katika masuala ya mazingira, Dk Richard Muyungi, amethibitisha hili na kueleza kuwa fedha hizo zinahitajika kama ufadhili na si mkopo.

Hata hivyo, hakueleza ni kwa jinsi gani fedha hizo zitawafikia wakulima moja kwa moja, suala ambalo ndilo kiini cha mashaka ya Nsimadala na wakulima wengine wa Tanzania.

Kwa mujibu wa EAFF, pengo la fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima wadogo wa Afrika Mashariki ni kubwa. Takwimu zinaonyesha mwaka 2021, fedha zilizowafikia wakulima wa chini zilikuwa asilimia 0.51 ya kile kilichohitajika.

Hali hiyo ndiyo inayowapa hofu wakulima kuwa huenda fedha mpya za COP30 zikapitia ngazi zote za kimataifa na kitaifa bila kuwafikia wale wanaohangaika kila msimu.