Wanachuo wanaodaiwa kujeruhi wakigombea mwanaume wana kesi ya kujibu

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewakuta na kesi ya kujibu wanafunzi watatu wa vyuo vikuu jijini Dar es Salaam, wanaokabiliwa na kesi ya jinai wakidaiwa kutenda makosa wakigombania mwanaume.

Wanafunzi hao ni Mary Matogolo (22), mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ryner Mkwawili wa Chuo Kikuu Ardhi na Asha Juma, wa Chuo cha Uhasibu, Dar es Salaam (TIA).

Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga, wanakabiliwa na jumla ya mashtaka manane.

Wanadaiwa kumsababishia madhara kimwili mwanafunzi mwenzao, Magnificant Kimario, kutishia kuua, kutoa taarifa za uongo mitandaoni na uharibifu wa mali.

Jamhuri katika kuthibitisha mashtaka hayo iliwaita mashahidi 10, akiwamo mwathirika, Magnificant na baada ya kufunga ushahidi wake jana Ijumaa, Novemba 21, 2025, mahakama katika uamuzi iliridhika kuwa washtakiwa wana kesi ya kujibu.

“Mahakama baada ya kuzingatia ushahidi wa upande wa mashtaka, imeridhika kuwa washtakiwa wote mna kesi ya kujibu,” amesema hakimu.

Hakimu Mwankuga ametoa uamuzi baada ya mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Gabriel Kamugisha kueleza baada ya kuwaita mashahidi 10 hawatakuwa na shahidi mwingine, hivyo kufunga kesi ya upande wao.

Kwa uamuzi huo, washtakiwa wanaowakilishwa na wakili Peter Shapa, wanapaswa kujitetea. Hakimu Mwankuga ameamuru waanze kutoa utetezi wao Jumatano, Novemba 26, 2025.

Washtakiwa walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Mei 30, 2025 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Tumaini Mafuru.

Kabla ya kupandishwa kizimbani walikamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi baada ya kipande cha picha mjongeo (video clip) kusambaa mitandaoni Aprili 20, 2025, ikidaiwa walishiriki kumdhalilisha mwanafunzi mwenzao.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote wanadaiwa Machi 16, 2025, eneo la Sinza, wilayani Ubungo walikula njama kwa nia ya kutenda kosa la kuchapisha taarifa za uongo.

Shtaka la pili linawakabili Mary na Asha wanaodaiwa siku hiyohiyo walisambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa WhatsApp yenye maneno: “Toa sauti umefanya mapenzi na Mwijaku lini na wapi.”

Ryner, katika shtaka la tatu anadaiwa siku hiyohiyo alisambaza taarifa ya uongo kupitia mtandao wa WhatsApp.

Shtaka la nne la kusababisha madhara linamkabili Mary anayedaiwa siku hiyohiyo alimshambulia Magnificant Kimario kwa kumpiga kichwani kwa chuma na kumsababishia maumivu makali.

Washtakiwa wote katika shtaka la tano wanadaiwa kwa kutumia nguvu walimvuta nywele Magnificant na kumsababisha madhara makubwa.

Katika shtaka la sita na la saba, Mary anadaiwa kuharibu laini ya simu na simu aina ya Samsung yenye thamani ya Sh700,000, mali ya Magnificant.

Shtaka la nane linawakabili washtakiwa wote wanaodaiwa walitishia kumuua Magnificant kwa kutumia kisu.

Washtakiwa wote wamekana mashtaka hayo na wako nje kwa dhamana.