Yanga imeibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kwanza hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ikiifunga AS FAR Rabat kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Katika mechi hiyo ya Kundi B lenye timu zingine za JS Kabylie na Al Ahly, Prince Dube ndiye aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 56.
Kabla ya kufungwa bao hilo na Yanga kupata ushindi huo, rekodi zinaonyesha timu hiyo hii ni mara ya sita inacheza hatua ya makundi michuano ya CAF ndani ya kipindi cha miaka kumi kuanzia 2016, na zote hizo inaanza na timu zenye asili ya Waarabu.
Katika mechi tano zilizopita dhidi ya Waarabu kabla ya kukutana na AS FAR Rabat, Yanga ilipoteza zote, hali iliyomfanya Kocha Pedro Goncalves kuingia uwanjani na mtihani wa kuvunja rekodi hiyo mbovu kwa kikosi hicho.
Si kupoteza tu, bali Yanga mechi hizo haikufanikiwa kufunga bao lolote ukiwa ni mtihani mwingine kwa Pedro, kwanza kufunga bao, pili kutopoteza mbele ya Waarabu kwenye mechi ya kwanza ya kundi michuano ya CAF. Kweli amefanikiwa.
Prince Dube ndiye aliyemaliza kila kitu baada ya kufunga bao pekee dakika ya 58 na kuifanya Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Kabla ya kucheza na AS FAR Rabat, Yanga ilianza Juni 19, 2016 ambapo ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika, mechi ya kwanza ya kundi ikifungua na MO Bejaia ya Algeria, ikapoteza kwa bao 1-0.
Mei 6, 2018, Yanga ilishiriki Kombe la Shirikisho na hatua ya makundi ilianza dhidi ya USM Alger kutoka Algeria, ikapoteza kwa mabao 4-0.
Msimu wa 2022-2023, Yanga ilianzia Ligi ya Mabingwa, lakini ikaangukia Shirikisho baada ya kutolewa na Al Hilal hatua ya pili, ikakutana na Club Africain, ikaitoa kwa jumla ya bao 1-0 na kufuzu makundi.
Hatua ya makundi, mechi ya kwanza ilikutana na US Monastir ya Tunisia na kupoteza kwa mabao 2-0.
Msimu wa 2023-2024, ilikuwa Ligi ya Mabingwa, mechi ya kwanza makundi ilikutana na Al Hilal ya Sudan na kufungwa 2-0, kisha 2024-2025, ilifungwa 3-0 na CR Belouizdad ya Algeria, ikiwa mechi ya kwanza hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa.
Yanga ilianza mechi kwa kasi lakini umakini wa safu ya ulinzi ya AS FAR Rabat ukawaokoa na presha ya kuruhusu bao la mapema.
Katika kuonyesha Yanga ilihitaji bao la mapema, ilifanya mashambulizi manne makali katika lango la AS FAR Rabat ndani ya dakika 10 za kwanza.
Kati ya mashambulizi hayo, matatu kutoka kwa Prince Dube akianza kuishughulisha safu ya ulinzi ya wapinzani dakika ya kwanza, ambapo Mohamed Hussein alipiga krosi, mshambuliaji huyo akaunganisha kwa kichwa, kipa Ahmed Reda Tagnaouti akaokoa na kuwa pigo la kona.
Pacome Zouzoua alipiga kona hiyo, Dube tena akapiga kichwa, kipa Ahmed Reda Tagnaouti akakaa imara na kuokoa tena hatari akiwa amesimama katikati ya mstari wa goli.
Haikuwa tu bahati kwa Dube, kwani dakika ya saba, alipokea mpira kutoka kwa Mudathir Yahya, baada ya kipa Ahmed Reda Tagnaouti kuokoa vibaya, lakini shuti alilopiga akiwa nje kidogo ya boksi, kipa huyo akadaka. Baada ya kosakosa hizo tatu za Dube, mashabiki wa Yanga wakaanza kupiga kelele wakiimba jina lake. Dube! Dube! Dube!
Celestine Ecua naye alifanya shambulio moja kwa AS FAR Rabat alipopiga kona iliyokuwa inakwenda moja kwa moja golini, lakini kipa Ahmed Reda Tagnaouti akaokoa tena.
Ndani ya dakika hizo kumi za kwanza, kipa wa AS FAR Rabat, Ahmed Reda Tagnaouti aliifanya kazi yake ipasavyo na kuiweka salama timu hiyo.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Yanga kuonekana kuitaka zaidi mechi tofauti na wapinzani wao walioingia na mfumo wa kujilinda zaidi kwani hawakufanya shambulio lolote la hatari hadi dakika 45 zinatamatika. Yanga ilifanya mashambulizi takribani matano yote ya hatari.
Kulikuwa na vita kubwa upande wa kushoto kwa AS FAR Rabat, ambapo beki, Tó Carneiro alikuwa akipambana na Celestine Ecua.
Yanga ilikuwa inautumia zaidi upande huo kupeleka mashambulizi kuliko kulia alipokuwa Pacome na kati alipocheza Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya.
Kipindi cha pili kilipotaka kuanza, Kocha wa AS FAR Rabat, Alexandre Miguel Crispin Dos Santos, alifanya mabadiliko ya wachezaji wawili. Aliwatoa Khalid Ait Ourkhane na Reda Slim, wakaingia Abdelfettah Hadraf na Hamza Kharba.
AS FAR Rabat ilisubiri hadi dakika ya 53 kufanya shambulizi langoni mwa Yanga ambapo krosi iliyopigwa na Youssef Alfahli, iliunganishwa kwa kichwa na Ahmed Hamouddan, lakini kipa wa Yanga, Djigui Diarra akakaa imara na kuzuia akidaka bila wasiwasi.
Dakika ya 56, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves akafanya mabadiliko ya kwanza kwa kumtoa Cestine Ecua na kuingia Edmund John.
Dakika mbili tu baada ya Edmund kuingia, Yanga ikapata bao lililofungwa na Prince Dube ambaye mpira alioupata upande wa kulia, akaingia nao hadi ndani ya boksi na kufunga.
Kuingia kwa bao hilo, kuliibua shangwe kubwa huku mashabiki wa Yanga wakiimba tena jina la mshambuliaji huyo. Dube! Dube! Dube!
AS FAR Rabat ambayo mwanzo ilionekana kukaa sana nyuma, bao hilo likawafanya watoke na kwenda kushambulia, lakini wachezaji wa Yanga walikaa imara.
Mabadiliko mengine aliyofanya Pedro ni dakika ya 65, alipomtoa Mudathir na kuingia Lassine Kouma. Dakika ya 82 akawatoa Prince Dube na Maxi Nzengeli, wakaingia Andy Boyeli na Mousa Balla Conte.
AS FAR Rabat nao wakafanya mabadiliko kwa kumtoa Ahmed Hammoudan na kuingia Soulaimane Elbouchqali, kisha Zineddine Derrag akampisha Habessi Achref.
Ushindi huo umeifanya Yanga kuwa na mwanzo mzuri wa mechi za makundi ya michuano ya CAF baada ya kushindwa kufanya hivyo tangu mwaka 2016 ambapo haikuwahi kushinda mechi ya kwanza.
Wikiendi ijayo, Yanga itakuwa Algeria kukabiliana na JS Kabylie katika mechi ya pili ya Kundi B katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Baada ya hapo, itasubiri hadi Januari 23, 2026 na Januari 30, 2026 kucheza dhidi ya Al Ahly, mechi mbili ikianzia ugenini kisha nyumbani.