USHINDI wa bao 1-0 dhidi ya Ceassia Queens umeipa jeuri Alliance Girls ambayo inaamini ni ishara njema kwa msimu huu, huku kocha msaidizi wa timu hiyo, Amani Lwambano akitaja kinachowapa ujasiri huo.
Alliance iliichapa Ceassia Queens ya Iringa katika mchezo wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara kwenye Uwanja wa Nyama-gana mjini Mwanza na bao pekee likifungwa na Yoranda Komba katika dakika ya 86.
Akizungumza baada ya ushindi huo, Lwambano alisema msimu huu huenda ukawa na mambo mazuri kwa timu hiyo kwa kuwa wamekuja na mikakati imara wakiboresha kikosi chao.
Alisema katika misimu ya nyuma walikuwa wakiwatumia wanafunzi wanaosoma katika shule zao kwa asilimia kubwa, lakini sasa wameamua kuchanganya kikosini kwa kuweka wachezaji wazoefu akiwemo kipa Husna Mtunda.
“Lengo letu ni kuendelea kushinda mechi na tunaamini hilo linawezekana kwa sababu tulikuwa tunatumia zaidi wana-funzi, lakini msimu huu kuna mabadiliko,” alisema Lwambano na kuongeza:
“Kuna mchanganyiko wa wachezaji wazoefu. Kwa hiyo tunaamini utakuwa msimu mzuri kwetu kwa sababu tumelenga kumaliza katika nafasi nne za juu.”
Akizungumzia mchezo dhidi ya Ceassia Queens, Lwambano alisema zilikuwa dakika 90 ngumu kwao akiwapongeza wachezaji kwa kupambana hadi dakika ya mwisho na kupata alama tatu.
“Tunashukuru tumeanza msimu vizuri na ili tumalize katika nafasi za juu lazima tupate matokeo kwa timu ambazo ziko kwenye kiwango sawa na chetu,” alisema Lwambano.