TIMU ya Azam imeanza vibaya mechi za Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kufungwa mabao 2-0 na AS Maniema Union, katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Stade des Martyrs, huko jijini Kinshasa DR Congo.
Katika mechi hiyo ya kwanza, licha ya Azam kumiliki mpira kwa asilimia 58, kipindi cha kwanza, ila wenyeji walitumia vyema nafasi ya bao la kuongoza la dakika ya 43, kupitia kwa Christian Balako, akipokea pasi ya Clement Pitroipa.
Hata hivyo, kipindi cha pili Azam ilianza mechi hiyo kwa kutengeneza mashambulizi ingawa ilikosa utulivu wa kumalizia nafasi kupitia kwa mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Jephte Kitambala, aliyekuwa anapambana na waajiri wake wa zamani.
Wakati Azam ikicheza kwa kushambulia lango la wapinzani wake kwa lengo la kusawazisha bao hilo, ila Maniema ilicheza kwa tahadhari kubwa na kutengeneza mashambulizi ya kushtukiza, ambapo dakika ya 85, ilipata bao la pili lililowahakikishia ushindi.
Bao hilo lilifungwa na Chadoma Ozome, akiunganisha vizuri mpira wa kichwa uliopigwa na Tshitenge Lusala na kumshinda kipa, Zuberi Foba, ikiwa ni timu ya pili ya Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu kupoteza.
Singida Black Stars juzi inayoshiriki pia kwa mara ya kwanza michuano ya CAF, kuchapwa ugenini mabao 2-0 na CR Belouizdad ya Algeria.
Baada ya kichapo hicho, Azam kwa sasa inarejea nyumbani kujiandaa na mechi ya pili ya hatua ya makundi dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, itakayopigwa Ijumaa hii ya Novemba 28, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
Azam iliyofika hatua ya makundi ya CAF kwa mara ya kwanza katika historia tangu klabu hiyo iasisiwe rasmi mwaka 2004, iko kundi B, sawa na AS Maniema Union ya DR Congo, Wydad Casablanca ya Morocco na Nairobi United ya Kenya.
Katika mechi nne zilizopita za CAF, Azam ilikuwa haijaruhusu bao lolote, ingawa rekodi hiyo imevunjwa na Maniema, baada ya kuanza kwa kuitoa EL Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 4-0, kisha kuichapa KMKM ya Zanzibar jumla ya mabao 9-0.
Kwa upande wa Maniema, iliitoa Pamplemousses ya Mauritius kwa jumla ya mabao 4-3, kisha hatua iliyofuata ikaitoa Royal Leopards ya Eswatini kwa penalti 4-3, baada ya mechi baina ya miamba hiyo kuisha kwa sare ya kufungana jumla ya mabao 2-2.
Kikosi cha Azam kilichoanza: Zuberi Foba, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Fuentes Mendoza, Yoro Diaby, Yahya Zayd, Himid Mao, Abdul Suleiman ‘Sopu’, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Idd Seleman ‘Nado’, Japhte Kitambala.