Bodaboda Njombe waonywa uchochezi | Mwananchi

Njombe. Jeshi la Polisi mkoani Njombe limewataka madereva wa bodaboda wilaya ya Njombe kutumia vizuri mitandao ya mawasiliano ya simu na mingineyo katika kujipatia kipato na kuacha kusambaza taarifa za uchochezi zinazoweza kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani nchini.

Hayo yamesemwa leo Novemba 23, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza na waendesha Bodaboda wa Wilaya ya Njombe katika mkutano uliofanyika viwanja vya jeshi hilo wilayani Njombe.
Amesema hakuna aliyefurahia yale yaliyotokea Oktoba 29,2025, kwa kuwa walioumia ni Watanzania wote wakiwemo askari pamoja na wananchi bila ya kujali itikadi zao.
“Wapo askari waliopata majeraha ,vilema na kuna wengine wamefariki, lakini pia wapo raia na wenyewe wamepata vilema na wengine wamefariki na wapo raia wengine mali zao zimeharibiwa,” amesema Banga.

Amesema Mkoa wa Njombe ni wachapakazi hivyo bodaboda hawana sababu ya kushinda kwenye mitandao na kutukana watu badala yake wafanye kazi ili kuingiza kipato kwa ajili manufaa yao na familia zao kwa ujumla.

Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Mkoa wa Njombe (RCO), Joseph Malongo amesema madereva bodaboda wana jukumu la kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa kuwa wao wanasafirisha abiria wa aina mbalimbali kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Wakati mnabeba hao watu kuna wengine wazuri wachache wana matatizo yao ya uhalifu na huyo anaweza kuleta madhara kwa jamii” amesema Malongo.

Mwenyekiti wa Bodaboda wilayani humo,  Velmund Msigwa amesema   wana vituo 76 ndani ya wilaya hiyo na kila mwanachama wao ana utambulisho wake na namba na kila kituo kina mwenyekiti, hivyo ameshatoa maelekezo na hakuna mwanachama atakayetumia vibaya mitandao ya kijamii atakayefanya hivyo atafutiwa uanachama.

“Nimeshawapa maelekezo hakuna mwanachama yeyote atakayeruhusiwa kutumia vibaya mitandao ya kijamii akibainika hatakuwa na hadhi ya kuwa mwanachama na stahiki zake zote zitapotea” amesema Msigwa.

Mmoja ya madereva wa bodaboda wilayani humo,  Kelvin Ngulo ameliomba Jeshi la Polisi kutoa ushirikiano kwa madereva bodaboda pindi kunapotokea uhalifu kwa kuacha kukamata hata wasiohusika.

“Mtu ametoka Mng’ate huko siyo bodaboda lakini amefanya tukio hapa inaonekana ni watu wa hapa naomba busara zitumike mnapoingia kwenye operesheni na kuacha kukamata watu bila ya utaratibu” amesema Ngulo