:::::::
Bondia Mtanzania, Pius Mpenda ameweka historia katika pambano la kimataifa lilifonyika jijini Riyadh katika nchi ya Falme za kiarabu baada ya kumlazimisha sare Mmexico, Julio Ruiz.
Mpenda ameweka historia hiyo mbele ya maelfu ya mashabiki wa mchezo wa ngumi waliojitokeza kushuhudia pambano hilo ambalo limefanyika katika ukumbi wa ANB Arena uliopo jijini Riyadh.
Katika pambano hilo la raundi sita Mpenda alianza kwa umakini mkubwa wa kumsoma mpinzani wake Ruiz ambaye kimo chake ni mrefu kuliko Mtanzania huyo kitendo ambacho kilimpa urahisi bondia Mmexico kufanya mashambulizi akiwa mbali.
Kadri muda ulivyozidi kwenda ndipo Mpenda akabadili mbinu akaacha kujilinda zaidi kama alivyofanya kwenye raundi za awali na kuanza kucheza kwa kuingia ndani na kuanza kumtupia makonde Ruiz ambaye muda mwingi alikua akishambulia na kuacha eneo lake la tumbo na mbavu kubaki wazi.
Mpenda alikua akipiga ngumi za mahesabu ambazo nyingi zilikua zikitua mahala sahihi huku Ruiz na yeye akishambulia hivyohivyo lakini baadhi ya ngumi zake zikipenya usoni na zingine kutuma kwenye ‘guard’ ya bondia huyo kutoka Tanzania.
Ilipofika raundi ya tano Mpenda alimmudu vizuri Ruiz na kumtandika ngumi kali ambapo moja ilitua katikati ya jicho na sikio la kushoto, ngumi nyingine zikimpeleka hadi kwenye kamba kitendo ambacho wasaidizi wake waliokua kwenye kona yake walizidi kumpa mbinu bondia huyo wa Tanzania kucheza huku akiwa jirani zaidi na Mmexico hiyo.
Baada ya kutamatika kwa raundi ya sita pambano liliisha na matokeo yakiwa ni sare ambayo Mpenda ameipata kwa haki kutokana na kuonesha mchezo mzuri kwenye ardhi ya ya ugenini.
Mpenda ni bondia namba tatu nchini Tanzania kati ya mabondia 36 akiwa na nyota moja na nusu huku Duniani akiwa wa 223 kati ya 1934 katika uzani wa ‘middle weight’ akicheza mapambano 17 akishinda 11 akipoteza manne na kutoka sare mapambano mawili.
Na kwa upande wa Ruiz ni bondia namba nne nchini Mexico kati ya mabondia 152 na Duniani ni wa 50 kati ya 1,820 akiwa na nyota tatu akicheza mapambano 14 akishinda 13 na sare pambano moja dhidi ya Mpenda alilocheza leo.
