CHUO cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (FDC Kibaha) kimesema kinajvunia kuendelea kukuza ujuzi wa kazi kwa vijana pamoja na kuboresha miundombinu kwa gharama ya Sh. milioni 860 ambazo zimetolewa na Serikali.
Akizungumza leo Novemba 22,2025 wakati wa mahafali ya 53 tangu kuanzishwa kwa Chuo hicho Mkuu wa Chuo Joseph Nchimbi ametumia nafasi hiyo kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika kukuza ujuzi kwa vijana nchini.
Nchimbi aliyekuwa akizungumza kuhusu Chuo hicho mbele ya mgeni rasmi Elisante Ngure,amesema Kibaha FDC ni mahali pa kutengeneza vijana wa kazi, wenye ujuzi na maarifa.
Akieleza zaidi Nchimbi amesema chuo hicho kilianzishwa mwaka 1964 kama Farmers Training Centre chini ya ushirikiano wa Serikali ya Tanganyika na nchi za Nordic.
“Baada ya mwaka 1970, mradi huo ukawa chini ya Shirika la Elimu Kibaha, kisha mwaka 1975 kikabadilishwe kuwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (FDC).
“Kwa miongo hiyo, Kibaha FDC kinatajwa kama chuo mama nchini, kwa kuwa kimetoa wataalamu na walimu waliokwenda kusimamia uanzishaji wa vyuo vingine vya Maendeleo ya Wananchi kote Tanzania,”amesema Nchimbi.
Kuhusu mafunzo yanayotolewa katika chuo hicho amesema yamejikita kwenye ujuzi wenye mahitaji makubwa sokoni, huku wanafunzi wakifanya mitihani ya VETA kupata vyeti vinavyowawezesha kuajiriwa au kujiajiri.
Ameongeza pia mafunzo yanayotolewa yanamhakikishia kijana kujiamini na kujiendeleza, uzalendo, ujasiriamali,maarifa ya TEHAMA pamoja na stadi za maisha na mawasiliano.
Akizungumzia wahitimu amesema mwaka huu wamehitimu 112 ambako kati yao wanaume ni 79 na Wanawake 33.”Wamehitimu wamemaliza katika fani sita za umeme, ufundi magari, ufundi pikipiki, Umeme,Useremala,Mifumo ya Kompyuta pamoja na fani nyingine za ufundi.
Kwa upande wa mafanikio amesema Chuo kimepata mafanikio kadhaa yakiwemo kupokea Sh. milioni 860 kwa ukarabati wa miundombinu, Ujenzi wa uzio kwa kushirikiana na wazazi.
Pia uwepo wa kozi fupi zaidi ya 10 kwa njia ya mtandao (online) kupitia ruzuku ya TEA, ambapo watu 6,145 wamenufaika bure.
Aidha kutoa wahitimu wanaoajiriwa na kujiajiri kwenye sekta za viwanda, maji na umeme.Wanachuo kushiriki katika miradi ya ujenzi wa Shirika la Elimu Kibaha ikiwemo mabweni na madarasa.
Kuhusu changamoto,Nchimbi amesema kumekuwepo na tabia ya Wanachuo kuacha masomo kutokana na gharama au kupata ujuzi mapema, ukosefu wa gari maalum la chuo pamoja na kukosa ruzuku ya chakula kwa wanafunzi.
Katika kukabiliana na changamoto hizo Chuo kinapendekeza Wanafunzi wasioweza kumudu gharama wapewe ushauri wa kuchagua kozi fupi.Ushirikiano uendelee na Shirika la Elimu Kibaha katika matumizi ya magari na Serikali ifanyie kazi ombi la ruzuku ya chakula.
Aidha Nchimbi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha ukarabati wa chuo, huku akiipongeza Bodi ya Chuo inayoongozwa na Dkt. Rogers Shemwelekwa (Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha) kwa mchango wake katika maendeleo ya chuo.
Bw. Elisante Joackim Ngure aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 53 ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (FDC Kibaha),mkoani Pwani.
Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (KIBAHA-FDC), Bw. Joseph Nchimbi.akisoma hotuba yake wakati wa mahafali ya 53 tangu kuanzishwa kwa Chuo hicho.
Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (KIBAHA-FDC), Bw. Joseph Nchimbi (kushoto) akilisha keki Bw. Elisante Joackim Ngure aliyekuwa mgeni rasmi wakati mahafali ya 53 tangu kuanzishwa kwa Chuo hicho.
Bw. Elisante Joackim Ngure aliyekuwa mgeni rasmi wakati mahafali ya 53 tangu kuanzishwa kwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha akimlisha keki mwakilishi wa wanafunzi.
Mwakilishi wa wazazi na walezi akitoa neno la shukurani wakati wa mahafali ya 53 ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (FDC Kibaha),mkoani Pwani.