BAADA ya kupoteza mechi sita za Ligi Kuu Bara, kocha wa KMC, Marcio Maximo amesema timu hiyo inapaswa kuanza kulikodolea macho dirisha dogo la usajili la Januari, 2026 ili kuboresha kikosi.
Ingawa kocha huyo katika mazungumzo yake na Mwanaspoti alidai baada ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa JKT Tanzania juzi, anauona mwanga wenye matumaini kutoka kwa wachezaji waliopo, lakini haiepukiki kuanza kufikiria kuongeza wachezaji wengine.
Bao la kipindi cha pili lililotokana na krosi ya Anuary Kilemile katika dakika ya 61 kisha ikambabatiza beki wa KMC, Ibrahim Abbas ‘Nindi’ lilitosha kuamua mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa KMC Complex.
Licha ya kuwa na mwendelezo wa matokeo mabovu, Maximo alisema anaona mabadiliko kidogo kwenye kikosi kwani mchezo huo walicheza vyema, lakini hawakupata matokeo mazuri.
Alisema usajili ndilo hitaji kubwa ambalo linatakiwa kufanywa kwa haraka, kwani kuna maeneo bado yanavuja.
“Tumepoteza mechi nyingine ambayo tumecheza vizuri. Zipo mechi nne tumeonyesha kiwango bora, lakini tumepoteza. Nadhani ni wakati wa kuangalia namna tutakavyoboresha kikosi chetu,” alisema kocha huyo.
“Tuna dirisha dogo (la usajili) linakuja. Ni wakati wa kuanza kufikiria nguvu gani tutaweza kuiongeza ili ije kubadilisha mambo. Tunahitaji kuleta watu ambao watatuongezea thamani uwanjani. Tunatengeneza nafasi, lakini tunashindwa kuzitumia.”
KMC ambayo inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi imepoteza mchezo wa sita, huku ikishinda mechi moja kati ya saba ilizocheza. KMC itashuka uwanjani Jumanne, Novemba 25, saa 10:00 jioni katika Uwanja wa KMC Complex.