Mtanzania aingia kikosi bora CAFWCL

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limetoa orodha ya kikosi bora cha mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Mtanzania Hasnath Ubamba anayekipiga FC Masar ya Misri akiwemo ndani.

Siku chache zilizopita As Far Rabat ya Morocco ilinyakua ubingwa wa michuano hiyo iliyoanza kupigwa Novemba 08 hadi 21, baada ya kuitandika Asec Mimosas ya Ivory Coast mabao 2-1 kwenye fainali iliyopigwa Uwanja wa Suez Canal Ismailia, Misri.

Kwa upande wa chama la Ubamba lilimaliza nafasi ya nne baada ya kutolewa nusu fainali ikichapwa bao 1-0 dhidi ya Asec, ikaanguka kutafuta nafasi ya mshindi wa tatu na  ilitandikwa mabao 3-1 na TP Mazembe.

Baada ya mashindano hayo kutamatika CAF ilitoa kikosi bora cha mashindano na Ubamba ameingia kwenye listi ya nyota 11 waliofanya vizuri msimu huu.

CAF 01


Kwenye mechi zote tano winga huyo alicheza sawa na Mtanzania mwenzake anayecheza nafasi ya beki wa kati, Violeth Nickolaus aliyejiunga msimu huu akitokea Simba Queens.

Katika mechi tano Ubamba alifunga mabao mawili na asisti moja, akinyakua tuzo moja ya Woman of the Match kiwango ambacho kimemfanya aingie kwenye kikosi bora cha msimu.

Akizungumzia kiwango chake Ubamba amesema “Ni kufuata maelekezo ya kocha tu ndiyo kumefanya niwe hivi pamoja na kushirikiana na wenzangu, safari yangu bado, ndiyo kwanza naanza na naendelea kujifunza vingi lakini ni jambo la kumshukuru Mungu.”