Mtu wa Mungu tumsifu Yesu Kristu, nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai. Ni imani yangu kuwa kwa neema ya Mungu unaendelea vizuri wewe na familia yako. Namtukuza Mungu kwa kukupa kibali tena siku ya leo kutafakari pamoja nami ujumbe wa leo ambao ninajua kwa hakika utakubariki na kugusa maisha yako.
Leo tutajifunza kwa habari ya uchungu. Uchungu ni maumivu ya ndani anayopata mtu baada ya kupitia changamoto mbalimbali.
Uchungu unaweza kusababishwa na mambo mabaya madogo madogo anayofanyiwa mtu. Mrundikano wa mambo hayo mabaya unaweza kupelekea mtu kuwa na maumivu ndani ya moyo wake.
Pia dharau, masimango, kuonewa, manyanyaso na mengine mengi kama hayo yanapozidi kwa mtu huweza kusababisha maumivu na hatimaye kuweka uchungu ndani ya moyo wake. Wengi wetu tumepitia maumivu tofauti tofauti, kazini, kwenye ndoa, katika familia, wazazi wengine wana uchungu juu ya watoto wao. Baadhi yetu kwa neema ya Mungu tumeweza kuvuka lakini wengine bado wanapitia maumivu makali ndani ya mioyo yao.
Hana mke wa Elkana alipitia maumivu kutokana na manyanyaso kutoka kwa Mke mwenzie, manyanyaso hayo na masimango vilisababisha maumivu ndani ya moyo wake kwa sababu Mungu alikuwa amefunga tumbo (hakuwa na mtoto). Uchungu aliokuwa nao ulikuwa mzito kiasi ambacho hakuweza kula, alikuwa mtu wa kulia tu maumivu ndani yake yalikuwa makali sana, moyo ulijaa huzuni na uchungu.
1Samweli: 1:10-16 “Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana akalia sana” mstari wa 13. Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa.
2 Wafalme: 4 ni habari za mwanamke Mshunami, aliyekaa muda mrefu pasipo kupata mtoto, kutokana na ukarimu wake Mungu anamkumbuka na kumpatia mtoto, kwa bahati mbaya mtoto huyu anafariki na mama huyu anapata uchungu kwa kumpoteza mtoto wake. Maumivu ndani ya moyo wake ni makubwa kiasi ambacho anapofika kwa mtu wa Mungu analitambua hilo, Mstari wa 27. “Naye alipofika kwa Yule mtu wa Mungu kilimani alimshika miguu. Gehazi akakaribia amwondoe; lakini mtu wa Mungu akamwambia mwache; maana roho yake ndani yake ina uchungu”.
Kuna mahala ambapo Ayubu alipita, palikuwa pagumu sana, alikuwa mcha Mungu, Mungu alijivunia yeye lakini shetani alimjaribu. Ayubu alipoteza kila kitu, namaanisha kila kitu. Mali, watoto, kusalitiwa na mke wake hata rafiki zake walikuwa kinyume chake. Maumivu ya Ayubu hayakuvumilika, moyo ulichoka, huzuni ikatanda, uchungu ukamzidi.
Ayubu: 6:2-3. Ayubu anasema “Laiti uchungu wangu ungepimwa, na msiba wangu kutiwa katika mizani pamoja! Kwa kuwa sasa ungekuwa mzito kuliko mchanga wa baharini.”
Ayubu anafika mahala anatamani hata mtu apime kiasi cha uchungu alionao, maumivu yalikuwa makubwa, haikuwa rahisi kwake, pasipo neema ya Mungu hangeweza kuvuka. Aliendelea kumtumainia Mungu hata katika nyakati ngumu alizopitia na Mungu alimpa ushindi wa kurejeshewa kila kitu alichokuwa amepoteza.
Kila mmoja kutokana na maisha ya hapa duniani anajua moyoni mwake uchungu alionao huenda haupimiki, ni sawa na mchanga wa baharini kama ilivyokuwa kwa Ayubu. Natamani niseme na wewe ya kwamba Mungu yuko upande wako, jitie nguvu katika Kristo uwe na moyo mkuu utalivuka hili. Ndugu yangu akanipigia simu anasema “Mdogo wangu magari matatu yameungua, maduka mawili yamevunjwa na kila kitu kimeibiwa, hapa nilipo sina nguvu niko ndani, sijui pa kuanzia” Unaweza ona ndugu huyu anapitia wakati gani, anahitaji neema ya Mungu kuvuka mahala hapo.
Sijui ni kwa namna gani una uchungu ndani yako, lakini ni maombi yangu kwa Mungu kuwa yeye ambaye hakumwacha Ayubu, asikuache na wewe katika kipindi hiki, usiruhusu uchungu ulionao ukuzidi kiasi cha kumuasi Mungu, Mungu anajivunia wewe na anajua unaliweza hili kikubwa amini tu ya kuwa Mungu yuko upande wako na kamwe hawezi kukuacha.
Isaya:35:3 “Itieni nguvu mikono iliyodhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea” Nakusihi wewe mwenye nguvu, Mungu amekufanya kuwa salama si kwa ajili yako hapana, umesalimika ili uweze kuwaimarisha wale waliodhaifu, waliokata tamaa, wenye uchungu, waliokosa tumaini Mungu amejisazia wewe ili uwe baraka kwa mwenzako.
Luka: 22:40-43 Akapiga magoti akaomba akisema, “Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke (Malaika kutoka mbinguni akaja akamtia nguvu)”. Kuna mahala Yesu alifika akachoka, uchungu ukamzidi, akaomba na Mungu akaagiza malaika wakamtia nguvu. Faraja ya kweli inatoka kwa Mungu, anayeweza kurejesha amani ya moyo ulioumia, anayeweza kuponya majeraha ya ndani na kukuondolea uchungu ni Mungu. Ninakuombea katika Jina la Yesu Kristo aliye hai, Yule malaika aliyetumwa kumtia nguvu Yesu, Mungu amtume kwako pia leo hii ili arejeshe amani ndani ya moyo wako na uchungu wote ulionao uondoke katika Jina la Yesu na urejeshewe furaha. Haleluya
Mwalimu Peace Marino anapatikana Usharika wa KKKT – Ebeneza Nyashimo (Busega)
Kwa maombezi na ushauri: 0783999044.