Katika uhusiano wa ndoa, suala la kutotoshelezwa kimapenzi ni jambo linaloweza kumgusa mtu yeyote, na mara nyingi halimaanishi kwamba mwenzi wako hafai au hashughuliki.
Wakati mwingine, hata akiwa anajituma kadiri ya uwezo wake, bado unaweza kuhisi hakukati kiu ipasavyo. Hili si tatizo la mtu mmoja linawagusa nyote, hivyo haipaswi kulaumiana kwa namna yoyote ile.
Wanaume wengi hukosa kueleza karibu kile wanachokipenda, kile kinachowasha hisia zao, au namna wanavyotamani mambo yafanyike. Mwisho wa siku mke anajitahidi, lakini anabaki akifanya anavyodhani unataka, badala ya kufanya kile unachotaka kweli.
Kutokuwepo kwa mawasiliano ya wazi hutengeneza pengo ambalo baadaye huonekana mmoja kushindwa kukata kiu ya mwenzake.
Kuna kitu kwa upande wako hakipo sawa, pengine wakati unakutana naye unakuwa umelemewa na mawazo, uchovu na kutaka yeye afanye kila kitu bila kuwapo na uwazi wa nini hasa unataka. Hali ikiwa hivi ni ngumu kupatikana matokeo chanya.
Mwanaume aliyejaa mawazo mara nyingi hata akipewa mapenzi mazuri, haoni tofauti.
Hivyo pengine tatizo lipo kwako hali ya kimwili na kiakili haijakaa sawa.
Nilitamani ungenieleza kwa kirefu ilikuwaje huko nyuma hadi ukamuoa kama hali ilikuwa ni hii au imebadilika baadaye.
Pia kuna wakati hamu na kasi ya kimapenzi kati ya wanandoa huwa inatofautiana. Inawezekana wewe una nguvu au uhitaji mkubwa kuliko mke wako.
Tofauti za miili ni za kawaida. Lakini tofauti hizo zinahitaji mazungumzo ya utulivu, kwa ajili ya kueleweshana ili kupata muafaka wa pamoja. Mwanamke hawezi kuboresha kitu ambacho hajui muhusika ni wewe ambaye unajua hakukati kiu. Hivyo njia pekee ya kulitatua kwa sababu huyo ni mkeo utaishi naye kwa kadri mtakavyojaaliwa lazima mpate muafaka, njia pekee ya kulifanikisha hilo ni mazungumzo ya pamoja yatakayoegemea kumuelewesha nini unataka ili ukate kiu.
Muhimu wakati wa mazungumzo hayo uwe sahihi na yawe ya upole yenye vicheko na utani wa hapa na pale kuhakikisha hakuna anayemlaumu mwenzake kuwa hajui namna ya kuburudika au kuburudishwa.
Tofauti na hapo kauli yoyote isiyokuwa na staha kuhusu jambo hilo itampotezea kujiamini na pengine asiwe karibu na wewe kama zamani kwani yeye anaamini anakufurahisha na kukuburudisha kwa sababu hujawahi kumuelekeza cha kukufanyia.
Lakini unaweza kutumia busara kwa kumwambia… ‘ningependa tujaribu kuboresha upande fulani ili wote tufurahie zaidi’, anahisi kuwa ni sehemu ya timu, sio mtu anayeshutumiwa.
Kile ambacho mke anaweza kufanya ni kushiriki katika mazungumzo haya kwa utulivu, kukusikiliza bila kujihami, na kuwa tayari kujaribu njia au mbinu mpya mnapokubaliana.
Muhimu jichunguze je, huna msongo wa mawazo unapokutana naye, mwili na akili vipo sawa? Ukihakikisha upo sawa mazungumzo na mke wako yatakuwa rahisi, na suluhisho litapatikana na utakuwa mwarobaini wa kuishi na kiu ilihali bomba linalotoa maji unalo ndani.
Jambo la muhimu kuzingatia kuwa tayari kumfundisha unataka nini kwa njia ya staha, kama hujaridhika mrudishe mchezoni kwa namna mlivyokubaliana kwenye mazungumzo yenu. Usisahau naye ni mtu ana hisia na anachoka hivyo unatakiwa umrudishe mchezoni ili upate unachokitaka kwa usahihi.