Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma limekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni zikidai kuwa Padri Josephat Misigaro, Paroko wa Parokia ya Nguruka wilayani Uvinza, pamoja na wananchi wawili wanaofahamika kwa majina ya Vedasto na Selule, wametekwa na watu wasiojulikana. Polisi wamesema taarifa hizo ni za upotoshaji na hazina ukweli wowote.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma ACP Philemon Makungu, siku ya Jumamosi Novemba 22, 2025, padri huyo aliitwa Novemba 20, 2025 kwa mahojiano kuhusu tuhuma za kijinai, na baada ya mahojiano aliachwa huru.
Kuhusu wananchi wanaotajwa kutekwa, Polisi wamesema hakuna taarifa yoyote iliyoripotiwa kuhusu watu hao kupotea.
“Kuhusu Vedasto na Selule wanaodaiwa pia kutekwa, taarifa hiyo siyo ya kweli kwani hakuna taarifa iliyoripotiwa ya watu hao kupotea, hata hivyo endapo kuna mtu yeyote ambaye amepotelewa na ndugu au jamaa afike kituo chochote cha Polisi kuripoti ili ufuatiliaji ufanyike kumtafuta ndugu yake”, ameeleza.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma limewaomba wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati ufuatiliaji juu ya waliotoa na kusambaza taarifa hizo za upotoshaji ukiendelea, na likasisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika.
Related
