Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiwataka wananchi wenye ndugu na jamaa waliotoweka tangu vurugu za Oktoba 29, mwaka huu, kwenda kuripoti vituo vya polisi, imetoa hakikisho la usalama na amani kwa wananchi siku ya Desemba 9, 2025.
Aidha, imesema ipo katika mazungumzo na wadau mbalimbali wa maendeleo, kuwaeleza upande wa pili wa uhalisia wa yaliyotokea, huku ikijipanga pia kuhakikisha inatumia rasilimali za ndani kutekeleza miradi yake.
Kauli hizo za Serikali zinakuja baada ya kuibuka malalamiko ya wananchi wanaolalamikia kutoweka kwa ndugu na jamaa zao, na wengine wakidaiwa kufariki Oktoba 29, mwaka huu, lakini inakuwa vigumu kupewa miili yao.
Mzizi wa yote hayo ni tukio la maandamano yaliyozaa vurugu Oktoba 29 na 30, mwaka huu, na kusababisha vifo, uharibifu wa mali za watu binafsi na miundombinu ya umma.
Kutokana na matukio hayo, kumeibuka matamko mbalimbali ya jumuiya za kimataifa, likiwemo Bunge la Umoja wa Ulaya, lililopiga kura ya kusitisha misaada kwa Tanzania kwa kile kilichodaiwa kuwa Serikali imedhihirisha uvunjifu wa haki za binadamu.
Hayo yameelezwa leo, Jumapili Novemba 23, 2025, na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo la Oktoba 29.
Sehemu sahihi ya kwenda ni Polisi
Kuhusu ndugu waliopotelewa na jamaa zao, Msigwa alisema wanapaswa kwenda katika vituo vya polisi kutoa taarifa, kwa sababu ndiyo mamlaka inayoshughulika na masuala hayo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ndugu hao, ilichukua siku saba bila kupata miili ya ndugu na jamaa zao, ingawa walishapewa taarifa ya vifo vyao. Hali hiyo iliwaacha katika giza totoro.
Viongozi wa hospitali za rufaa na taifa walikiri kupokea miili ya waliopoteza maisha kutokana na matukio hayo, ingawa hawakuwa tayari kuweka hadharani idadi yao kwa kile walichoeleza, ni mamlaka ya polisi kueleza hayo.
Hata Mwananchi ilipomtafuta Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camilius Wambura Novemba 6, mwaka huu ili kujua idadi ya waliofariki na iwapo miili itakabidhiwa kwa familia zao, alijibu taarifa hiyo itatolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali (Gerson Msigwa).
Hata hivyo, leo Msigwa amesema “Kwa hatua hii, sehemu sahihi ya kwenda ni Polisi, kwa sababu ndiyo watu wanaoweza kufanya jitihada za kuwatafuta waliopotea. Kwa sasa siwezi kuwa na majibu kwa sababu matukio yalitokea wakati wa vurugu baada ya uchaguzi.”
Amesisitiza mwananchi yeyote, inapotokea ameona ndugu au jamaa yake haonekani, ahakikishe anakwenda polisi kutoa taarifa kwa hatua zaidi.
Msigwa ametumia jukwaa hilo kuwahakikishia wananchi kuwa hakutatokea vurugu siku ya Desemba 9, mwaka huu, kwa sababu vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kudhibiti.
Amesema pamoja na hamasa na uchochezi unaoendelea katika mitandao ya kijamii, Serikali inawahakikishia wananchi usalama na amani siku hiyo na kwamba wasiwe na wasiwasi.
Hata alipoulizwa iwapo sherehe za uhuru zitafanyika siku hiyo, amesema siku mbili baada ya jana, taarifa rasmi kuhusu tukio hilo la sherehe zitatolewa na Serikali.
Kuhusu wadau wa kimataifa
Katika mkutano huo, Msigwa amesema tangu kutokea kwa vurugu hizo kumekuwa na matamko ya baadhi ya wadau wa maendeleo, wakiweka msimamo wa kusitisha misaada kwa Tanzania, akisema Serikali ipo katika mazungumzo nao.
“Kumekuwa na matamko ya baadhi ya wadau wetu wa maendeleo na tunazungumza nao, na tunaamini hawana taarifa za upande wa Serikali. Tutawaeleza ya kwetu na watasema msimamo wao.
“Ni kweli kutakuwa na mtikisiko kwa watakaoshikilia msimamo, lakini Serikali itazungumza nao, na watakaoelewa bila shaka wataelewa, kwani hii sio mara ya kwanza wafadhili hao kusema maneno kama hayo,” amesema msemaji huyo wa Serikali.
Hata hivyo, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha itatumia njia nyingine kupata fedha za kutekeleza miradi yake, akisisitiza nchi haiwezi kuendeshwa kwa misaada pekee.
Novemba 14, mwaka huu, wakati akifungua Bunge la 13, Rais Samia Suluhu Hassan alieleza kusamehewa na kuachiwa huru kwa vijana waliojihusisha na maandamano kwa kufuata mkumbo na wakiwa mahabusu, lakini haikuonekana hadharani wakiachiwa hadi sasa.
Kuhusu hilo, Msigwa amesema maelekezo hayo ya Rais Samia yameshaanza kutekelezwa, na utekelezaji huo unafanyika taratibu na kazi ya kuwaachia inaendelea.
“Kazi hiyo inaendelea, na watu wanaachiwa taratibu taratibu. Mwisho wa siku, wataachiwa wote kwa mujibu wa ilivyoelezwa,” amesema Msigwa.
Alipoulizwa kuhusu idadi kamili ya waliopoteza maisha na kujeruhiwa, Msigwa amesema ni vigumu kutaja idadi yao kwa sababu tathmini inaendelea na tume inaendelea kuifanya kazi hiyo.
“Yeyote anayetoa takwimu ni mchochezi. Mwanahabari anahesabu vipi vifo? Tunapaswa kuwa na subira, na yaliyotokea hayakuwa mambo mazuri. Kila mmoja ana majonzi na masikitiko, tuwe watulivu, tathmini itafanyika na taarifa itatolewa,” amesema.
Kuhusu mpango wa fidia kwa waathirika, amesema yote hayo yatajulikana baada ya tume iliyoundwa kufanya uchunguzi itakapomaliza kazi yake na kutoa mapendekezo.
Pamoja na hayo, Msigwa ametoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na waliopata madhara ikiwemo kuumia, kupoteza mali, na kwamba Mungu ayaponye maumivu yao na awarejeshee walichokipigania na kukikusanya kwa jasho jingi.
“Tayari Rais Samia, baada ya kuapishwa, ameunda tume huru ya uchunguzi ambayo inaongozwa na Jaji mstaafu Mohamed Chande Othman. Ni muhimu kuwa na subira ili yote yaliyotajwa katika hadidu za rejea yatatolewa kwenye ripoti,” amesema.
Katika taarifa yake hiyo, ameonya vyombo vya habari vya kimataifa na wanaharakati wanaosambaza taarifa za matukio ya vurugu hizo bila kufuata misingi ya kitaaluma.
“Serikali au viongozi wa Serikali inasikitishwa na imeumizwa sana na matukio yale na madhara yake. Kuendelea kutangaza matukio yale au kupotosha au kuchochea kama ambavyo vyombo vya habari vya nje vinafanya haina msaada zaidi ya kuongeza maumivu,” amesema.
Ametoa wito kwa vyombo vya habari vya nje kuzingatia maadili na misingi ya uandishi wa habari na kuhakikisha usawa, haki na uwajibikaji wanapotoa taarifa.
Amehusisha kinachofanywa na wanaharakati na vyombo hivyo vya habari na kile alichokiita mpango wa makusudi wa kuharibu taswira ya Tanzania mbele ya dunia kwa maslahi ya kisiasa na kiuchumi.
“Wanatumia silaha ya kutumia simulizi mbaya inayoonesha nchi yetu ya hatari. Wanataka wageni, wakiwemo wawekezaji, wafanyabiashara, watalii na watu wengine wanaokuja kwa maslahi ya Tanzania, waogope ili tufe njaa,” amesema.
Amesema Tanzania kwa sasa ni moja ya nchi chache zinazopiga hatua za kiuchumi, na wengi hawaamini.
Amezitaja baadhi ya hatua hizo ni mpango wa ujenzi wa kilomita 160 za reli kwa ajili ya treni ya majini katika Mkoa wa Dar es Salaam, huku Dodoma ikiwa kilomita 105.
Kwa Dar es Salaam, amesema itaanza Kawe, Mwenye, Mlimani City, kisha Kariakoo, na kutakuwa na tawi kutoka Bibi Titi hadi Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.
Amegusia mafanikio katika ufanisi wa bandari nchini, na huduma za usafiri wa reli, barabara na anga.
Katika mkutano huo, pia amewaalika watalii kuendelea kutembelea Tanzania, akisema wanahakikishiwa ulinzi na usalama wao, hivyo wasiogope kuja nchini.