Tanzania yaanza vibaya Kombe la Dunia Futsal

TIMU ya taifa ya Wanawake Tanzania imeanza vibaya mechi zake za Kombe la Dunia la Futsal inayoendelea huko Ufilipino baada ya kupokea kichapo cha mabao 10-0 kutoka kwa Ureno.

Mechi hiyo ya Kundi C ilipigwa mapema asubuhi kwenye Uwanja wa Philsports Arena Pasig nchini Ufilipino.

Katika Futsal, mechi huchezwa kwa dakika 40 ambazo ni dakika 20 kwa kila kipindi. Kwa wastani wa muda huo, Tanzania imekubali kuchapwa bao moja kila baada ya dakika nne.

Katika mechi hiyo ya kwanza hatua ya makundi, Ureno ilionyesha utofauti mkubwa wa uzoefu, kasi na ubora wa kiufundi.

TANZ 01


Kuanzia filimbi ya mwamuzi, Ureno ilionekana kucheza kwa mpango mmoja wa kutawala mchezo, pressing ya juu, mabadiliko ya nafasi ya haraka, na utulivu wa kumiliki mpira kuliifanya Tanzania kushindwa kuhimili presha ya mechi hiyo.

Bao la mapema dakika ya tatu kupitia kwa nyota wa Ureno, Mariana Silva ambaye alikuwa mwiba mkali, liiivuruga safu ya ulinzi la Tanzania.

Hadi dakika ya 10, tayari walikuwa mbele kwa mabao 3–0, kitu kilichoiweka Tanzania kwenye presha ya kutafuta jinsi ya kuzuia mvua ya mashambulizi.

Licha ya jitihada za wachezaji wa Tanzania kujaribu kujipanga upya, walikosa mawasiliano, kujiamini kulipungua na walionekana kuchelewa kufanya uamuzi kwa haraka na kuwapa wenyeji mwanya wa kuongeza mabao.

TANZ 02


Kiwango cha mchezo wa futsal kinahitaji uamuzi wa sekunde, ubadilishaji wa kasi, na mzunguko wa wachezaji bila kuchoka. Tanzania ilionekana kuelemewa zaidi katika maeneo hayo yote manne, huku wakijilinda bila mpangilio na kuwaruhusu wapinzani kupata mashuti ya karibu mara kwa mara.

Baada ya mechi ya kwanza Tanzania itashuka tena kwenye Uwanja wa Philsports Arena Pasig kuumana na na New Zealand Novemba 26 na kumaliza makundi Novemba 29 ikiikaribisha Japan.