Usipuuzie maumivu ya kichwa, wataalamu watahadharisha

Dar es Salaam. Kama unapata maumivu ya kichwa yanayojirudia na huchukui hatua ya kumwona daktari bali unameza dawa tu, basi kiafya utakuwa unafanya makosa kwa kuwa, wataalamu wanasema si dalili njema.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, maumivu ya kichwa mara kwa mara ni dalili inayoashiria changamoto kwenye ubongo,  hivyo inahitajika ulazima wa kwenda hospitali.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu bilioni tatu ulimwenguni wanakabiliwa na maumivu ya kichwa yanayojirudia kama vile kipanda uso.

Pia, miongoni mwa athari zake maumivu ya kichwa yanaweza kuvuruga kazi, shule na maisha ya kila siku, hivyo  kusababisha kukosa shughuli kwa msongo wa mawazo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Novemba 23, 2025 Dk Fabian Maricha amesema kuumwa kichwa mara kwa mara kunaashiria shida kwenye mfumo wa ubongo.

“Sababu za kuumwa kichwa zipo za kimazingira, au kimwili lakini kuumwa mara kwa mara kama kipandauso inaashiria tatizo kwenye ubongo, ambalo linaweza kuletwa na unywaji wa pombe uliopindukia au mawazo yaliyokithiri.

“Ni ishara ya shida katika mwili au kwenye ubongo. Sababu za kichwa kuuma kwa kujirudia inaweza ikawa baadhi ya vyakula, baadhi ya dawa, lakini asilimia kubwa inakuwa inasababishwa na unywaji wa pombe, magonjwa, kemikali, mawazo, mazingira au ulaji wa mtu,” amesema.

Akieleza zaidi, Dk Maricha amesema ili kuepuka kuumwa kichwa mara kwa mara, kwanza ni muhimu kutokuwa na mawazo yaliyokithiri, kuzingatia ulaji mzuri, kufanya mazoezi na ukishagundua tatizo wahi kupate tiba mapema.

Amesema ukiwahi kupata matibabu unaweza kuokoa shida nyingine akitolea mfano shida ya macho kama maumivu ya kichwa ya mara kwa mara unayopata yanahusiana na mfumo wa macho.

Dk Maricha amesema inawezekana kichwa kinauma kumbe ni dalili ya shida ya macho, hivyo ukiwahi utapata tiba na kuepuka madhara yake ambayo yangeweza kujitokeza.

“Kwa kawaida kichwa hakiwezi kuuma bila sababu, bali kuumwa kwake ni ‘alert’ ya shida iliyopo,” amesema Dk Maricha.

Kwa mujibu wa WHO, maumivu ya kichwa ni miongoni mwa matatizo yanayoathiri sana mfumo wa neva, mwaka 2021, maumivu ya kichwa ya aina ya migraine yalishika nafasi ya tatu kwa kuleta mzigo mkubwa wa magonjwa ya neva DALYs (Disability-Adjusted Life Years).

Aina hizo za maumivu huleta maumivu, ulemavu, kupungua kwa ubora wa maisha na gharama za kifedha kwa mtu binafsi na jamii.

Kwa mujibu wa WHO, ni watu wachache duniani wanaopata utambuzi sahihi na matibabu stahiki kwa kuwa, tatizo la maumivu ya kichwa limekuwa likipuuzwa na kutokuwa na uangalizi wa kutosha.

Katika hatua nyingine, wataalamu wa afya wanaeleza hatua muhimu za kuchukuliwa ili kuepuka usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, ikiwamo kuacha matumizi ya dawa bila ushauri wa kitaalamu mtu anapohisi maumivu ya kichwa au sehemu nyingine ya mwili.

Mtaalamu wa famasia, Timothy Mbaga amesema sababu kuu za usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa.

Amesema mtu anapojitibu bila kufahamu anasumbuliwa na tatizo gani, huchangia kujenga usugu wa vimelea.

“Jambo lingine, unapoumwa hupaswi kujitibu, unapaswa kufanya vipimo na kufuata maelekezo ya daktari au mfamasia. Ukimpatia jirani dawa kwa sababu una dawa nyumbani, unamsababishia tatizo zaidi,” amesema Mbaga.

Pia, Mbaga amesema wapo wafugaji wanaowapatia mifugo dawa kisha kuuza maziwa bila kujua kuwa maziwa hayo bado yana mabaki ya dawa.

“Unapompatia mfugo dawa, hupaswi kutumia maziwa yake kwa siku 14, maziwa hayo yanapaswa kumwagwa si kutumika,” amesema.

Mfamasia Bingwa wa Binadamu, Samson Misinzo amesema usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni janga la dunia nzima na halizuiliki kirahisi.

“Wataalamu wanaongeza juhudi za kudhibiti tatizo hili, kwa sababu tunafahamu huko mbele linaweza kushindikana. Kulingana na takwimu za WHO, vifo milioni 1.1 hutokea kutokana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa,” amesema Misinzo.

Amesema vifo vinavyosadikika duniani kutokana na usugu huo ni milioni 4.7, huku nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara zikiathirika zaidi.

“Afrika huchangia vifo 250,000 kwa mwaka, na zaidi ya asilimia 60 vinatoka nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa Afrika Mashariki, tunapata takribani vifo 10,000 kwa mwaka vinavyohusiana moja kwa moja na usugu wa vimelea, na vifo vinavyosadikika kufikia 42,000 kwa mwaka (WHO, 2021),” amesema Misinzo.

Pia, amesema watoto chini ya miaka mitano wanaongoza kwa vifo nchini kutokana na tabia ya wazazi kuwapatia dawa bila ushauri wa kitaalamu.

Amesema ugonjwa wa nimonia umeonekana kuua watoto wengi zaidi kutokana na upungufu wa elimu kwa wazazi juu ya namna ya kuwahudumia watoto wanapougua.

“Katika kila vifo 100,000, vifo 980 vinahusu watoto chini ya miaka mitano. Hili ni tatizo kubwa, na wananchi wanapaswa kupewa elimu ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa. Tafiti zinaonesha kuwa kufikia mwaka 2050 huenda isiwezekane kupambana na tatizo hili,” amesema Misinzo.