Katika historia ya mwanadamu, malezi ya mtoto yamekuwa nguzo muhimu ya kuendeleza jamii.
Malezi hayo yamepitia mabadiliko makubwa kutoka kwa mfumo wa kijadi hadi wa kisasa, jambo ambalo limezua mjadala kuhusu ni aina ipi ya malezi inayofaa zaidi.
Je, malezi ya zamani hasa ya Kiafrika bado yana nafasi katika dunia ya sasa iliyokumbatia teknolojia, haki za binadamu, na maendeleo ya sayansi ya saikolojia?
Ili kufahamu kiini cha vita hii ya malezi ya usasa na uzamani, ni muhimu kuchambua kwa kina tabia, faida, na changamoto za kila upande.
Malezi ya zamani na maadili
Katika jamii za Kiafrika za kitamaduni, malezi yalizingatia misingi ya heshima, utiifu, maadili, mshikamano wa kijamii na kuishi kwa kufuata mila.
Watoto walilelewa si na wazazi pekee, bali na ukoo mzima. Hili liliimarisha nidhamu, ukarimu, na mshikamano miongoni mwa wanajamii.
Mfano wa mila iliyohimiza malezi bora ni jando na unyago, ambayo si tu iliwafundisha vijana kuhusu mabadiliko ya mwili, bali pia kuwajenga katika maadili, majukumu ya kijamii, na jinsi ya kuishi kwa staha na heshima.
Pia, katika baadhi ya jamii kama Wazulu au Wamasai, wazee walikuwa wakiheshimika kama hazina ya hekima na waliotoa mwelekeo wa malezi.
Aidha, katika familia nyingi za Kiafrika, adhabu ya kimwili ilionekana kama njia ya kawaida ya kuwaadhibu watoto. Lengo halikuwa kuwaumiza, bali kuwaongoza kwenye njia ifaayo. Watoto waliogopa kufanya makosa si tu kwa sababu ya adhabu, bali pia kwa kuhofia kuaibika mbele ya jamii.
Msomi wa falsafa na maadili, Profesa Raymond Mosha anasema zamani watoto walilelewa kama sehemu ya utamaduni mmoja chini ya wazazi na hata majirani.
‘’Tulilelewa na baba na mama, wasichana walizungumza na kina mama, wavulana walizungumza na kina baba. Mara nyingi watoto wanakuwa pamoja…mnafundishwa pamoja, mnafundishwa kwa methali, hadithi na zote hizo zilikuwa ni namna ya kufundisha maadili. Leo familia zetu zimevunjika hazipo kama zilivyokuwa…mambo ya Ulaya yamekuja huku kwetu, tunaona ya zamani hayana maana tena,’’ anasema.
Kwa upande mwingine, malezi ya kisasa yamejikita zaidi kwenye haki za mtoto, uhuru wa kujieleza, saikolojia ya ukuaji na matumizi ya teknolojia katika kujifunza.
Watoto wengi wa kizazi cha sasa huishi katika familia ndogo ambapo mlezi mkuu ni mzazi mmoja au wawili pekee. Teknolojia kama vile simu, televisheni na intaneti imechukua nafasi kubwa katika kukuza na kulea watoto, huku ikipunguza muda wa mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wazazi na watoto.
Malezi ya kisasa yanapinga vikali matumizi ya adhabu za kimwili, yakisisitiza zaidi mbinu za ushauri, kujenga uelewa wa ndani na mazungumzo.
Aidha, watoto wanapewa nafasi ya kutoa maoni yao, hata kuhoji baadhi ya maamuzi ya wazazi, jambo ambalo lilikuwa halikubaliki katika jamii za kale.
Licha ya maendeleo na mabadiliko yanayokuja na malezi ya kisasa, kuna sababu nyingi zinazofanya malezi ya Kiafrika ya jadi kuwa na umuhimu mkubwa hadi leo.
Kwa mujibu wa Profesa Mosha, ni lazima malezi ya zamani yaenziwe na kuchukuliwa kwenye mazingira ya sasa, hata kama hayatotekelezwa kama ilivyokuwa zamani.
Anaeleza: ‘’ Kama jamii tutayarishe vijana wanaofunga ndoa, wapate hata kozi ya mwaka ya mzima na wasichana hivyo hivyo’ Leo vijana wanaotaka kufunga ndoa hawatayarishwi kwa namna yoyote, hawaongei na wazee, hawapati chochote wanaenda kuoana tu baada ya siku mbili talaka.’’
Tuone faida nyinginezo; Mosi, kuimarisha maadili: Katika jamii nyingi za leo, kumekuwa na ongezeko la ukosefu wa maadili miongoni mwa watoto na vijana.
Malezi ya Kiafrika yalijenga maadili kupitia hadithi, methali, na mifano hai kutoka kwa wazee. Mfano, methali kama “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo” bado ina maana kubwa leo.
Kujifunza kupitia hekima za wazee huongeza maarifa na maadili kwa njia ambayo vitabu na mitandao haviwezi kutoa kwa ukamilifu.
Pili, kukuza mshikamano wa kijamii: Utamaduni wa “mtoto ni wa jamii” ulihakikisha kila mtu anahusika na malezi ya mtoto.
Hili linapunguza matatizo ya kisaikolojia kwa watoto na kuwajengea mazingira ya upendo na msaada.
Katika dunia ya leo ya utandawazi, ambapo watu wengi wanaishi mbali na familia zao, kuendeleza mfumo huu wa kijamaa kunaweza kusaidia kupunguza upweke na msongo wa akili kwa watoto.
Tatu, nidhamu na uwajibikaji: Watoto waliopitia mfumo wa malezi ya Kiafrika walijifunza mapema kuhusu majukumu yao katika familia na jamii.
Kazi za nyumbani, kusaidia katika shughuli za kiuchumi kama kilimo au ufugaji, na kushiriki kwenye matukio ya kijamii, kulijenga nidhamu na kuwafanya watoto kuwa na heshima ya kazi.
Nne, kuendeleza utamaduni: Mila kama hadithi za usiku, ngoma za asili, na sherehe za kimila zilisaidia kuhifadhi na kuendeleza utambulisho wa Kiafrika. Katika dunia ya sasa ambako vijana wengi wameathiriwa na tamaduni za Magharibi, kurudia baadhi ya vipengele vya malezi ya Kiafrika vyenye manufaa, kunaweza kusaidia kuhifadhi utambulisho wa Kiafrika.
Changamoto malezi ya asili dunia ya sasa
Hata hivyo, si kila kipengele cha malezi ya zamani kinaweza kutumika moja kwa moja katika dunia ya sasa. Baadhi ya changamoto za malezi ya zamani ni pamoja na ukandamizaji wa watoto. Mfumo wa “mzazi hana kosa” ulizima sauti za watoto, hata walipofanyiwa vitendo visivyofaa kama manyanyaso au ukatili.
Katika dunia ya sasa ambapo haki za watoto ni muhimu, kuna haja ya kuangalia upya eneo hili.
Kutokubalika kisheria kwa baadhi ya mila. Mila kama tohara ya wanawake (katika baadhi ya jamii), kulazimisha ndoa za utotoni, au kuadhibu kwa viboko vilivyozidi idadi si tu zina madhara kwa watoto bali pia zimepigwa marufuku kisheria katika nchi nyingi za Afrika.
Aidha, jamii nyingi za sasa hazihifadhi tena mfumo wa kijamaa. Mjini, watu wanaishi maisha binafsi na hawana muda wa kushiriki kwenye malezi ya watoto wa wengine.
Hii inaleta changamoto ya jinsi ya kuendeleza mila hizo katika mazingira haya mapya.
Suluhisho linaweza kupatikana kwa kuchanganya yale mazuri kutoka kwenye malezi ya jadi ya Kiafrika na yale ya kisasa kwa kufanya yafuatayo:
Mosi, kuhimiza maadili kupitia simulizi na methali, huku tukiwapa watoto nafasi ya kuuliza maswali na kuelewa kwa kina maana ya maadili hayo.
Pili, kutumia njia zisizo za kimwili katika kuwaadhibu watoto, lakini bado tukisisitiza umuhimu wa nidhamu.
Tatu, kuhimiza mshikamano wa familia na jamii, hata kupitia vikundi vya kijamii au mitandao, ili kila mtoto ahisi kuwa na nguzo ya msaada.
Nne, kuelimisha watoto kuhusu mila na tamaduni, huku tukitambua na kuachana na zile zilizopitwa na wakati au zinazokiuka haki za binadamu.
Kwa mawazo ya Profesa Mosha, tunaweza kuchukua tunu za zamani tukaziingiza kwenye mazingira ya kisasa.
‘’Kwa mfano, nimesema vijana wanaolekea kuoa na kuolewa watayarishwe mwaka mzima,’’ anaeleza.
Vita kati ya malezi ya usasa na uzamani si lazima iwe ya maangamizi au kuchagua upande mmoja.
Badala yake, inapaswa kuwa nafasi ya kutathmini, kuchuja na kuchanganya mazuri ya kila upande.
Malezi ya Kiafrika ya zamani yana hazina kubwa ya maadili, nidhamu, mshikamano, na utambulisho, ambayo bado yanafaa na yanahitajika katika dunia ya sasa.
Hata hivyo, ni muhimu kuyachakata kwa kuzingatia mazingira ya sasa ya kijamii, kielimu, na kisheria.
Kwa kufanya hivyo, tunaweza kulea kizazi chenye maadili mema, kinachoheshimu utamaduni wake na kuendana na mahitaji ya dunia ya sasa.