Dar es Salaam. Kutokana na mabadiliko ya teknolojia hasa katika uhifahdi wa taarifa (data), imeshauriwa watunza taarifa hizo mbali na kutumia mifumo ya uhifadhi ya seva pia wametakiwa kuwekeza kwenye mifumo mipya ya kisasa ya uhifadhi ya Cloud Storage.
Ikumbukwe taasisi, mashirika, kampuni au viwanda zinahifadhi taarifa zake kama mafaili ya ofisi, taarifa za wateja, programu au mfumo wa malipo katika mfumo wa uhifadhi kama kompyuta ya seva.
Seva ni mfumo wa utunzaji wa taarifa kwenye kompyuta maalumu ambayo inaendesha, kusimamia na kulinda data za watumiaji wengi kwa wakati mmoja. Seva huwa na uwezo mkubwa wa uhifadhi, kasi ya juu na mifumo ya usalama iliyoboreshwa kuliko kompyuta za kawaida.
Watumiaji hupata taarifa hizo kupitia kompyuta zao kwa kutumia jina la mtumiaji na nywila. Ikiwa seva iko kwenye data center, taarifa hulindwa dhidi ya hitilafu za umeme, moto na udukuzi.
Hata hivyo, gharama ya kununua matengenezo na kutunza vifaa (kwa seva za ndani) ni kubwa pia inahitaji wataalamu wa Tehama, kuathiriwa na hitilafu za vifaa kama diski au umeme.
Kwa upande wa Cloud Storage ni njia ya kuhifadhi taarifa hizo kidijitali ambapo inatumia seva zilizopo nje ya eneo la mtumiaji. Seva hizo huendeshwa na mtoa huduma wa tatu ambaye, kusimamia na kulinda data zote kwenye miundombinu yake.
Kupitia njia hii mtoa huduma huhakikisha taarifa zinaweza kupatikana wakati wowote kupitia mtandao wa intaneti. Kwa kutumia Cloud, taasisi au kampuni zinaweza kuhifadhi, kufikia na kudhibiti data bila kuwa na haja ya kujenga au kumiliki kituo chao cha data.
Hii hupunguza gharama za kununua vifaa na kuhamishia matumizi kwenye gharama za uendeshaji.
Cloud inatumia seva kuhifadhi taarifa kama mafaili, video, picha na taarifa za biashara. Mtumiaji hupakia (upload) data kupitia intaneti, na data hizo huhifadhiwa kwenye mashine pepe (virtual machine) ndani ya seva halisi.
Ili kuhakikisha upatikanaji wa kudumu na kuepusha upotevu wa data, watoa huduma hueneza data hizo kwenye virtual machines nyingi katika vituo tofauti vya data duniani ambapo mtumiaji anazipata kutumia tovuti, (browser), aplikesheni za simu.
Akizungumza mwishoni mwa juma kwenye warsha iliyowakutanisha kampuni ya Tehama ya Dynatech Solutions na wataalamu wa Tehama sekta ya uhifadhi taarifa (database), Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Exaud Kimboi, amesema kwa sasa teknolojia inarahisisha na kupunguza gharama hivyo wataalamu wanapaswa kuendana na kasi yake.
“Badala ya mtu kununua kopyuta kubwa na storage anaweza akaepuka gharama kwa kuweka taarifa zake kupitia Cloud kwa pesa kidogo, huko hakuna kukatika kwa umeme au intaneti, pia inaokoa muda na inapatikana mahali popote,” amesema.
Kimboi amesema sera ya nchi inataka kwa baadhi za taasisi taarifa zake ziwepo hapahapa nchini, lakini haizuii kujifunza mifumo mipya ya uhifadhi kutokana na mabadiliko ya teknolojia yaliyopo anaamini kama taifa tutaelekea huko.
“Rai yangu kwa kampuni na taasisi Tanzania ziandae watu kulingana na mabadiliko ya teknolojia kama Akili Unde (AI) na uhifadhi wa taarifa wa Cloud kwa kuwa zinahitaji maandalizi.”
Akieleza zaidi amesema kampuni inashirikiana na sekta ya elimu kwa wanafunzi kujifunza kuhusu Tehama ili wakimaliza chuo wawe na ujuzi unaohitajika kwenye soko.
Kwa upande wake, Rojas Mbara kutoka kampuni ya Jiko Express amesema uhifadhi wa Cloud ni mzuri ukilinganisha na miundombinu ya seva kwakuwa unapatikana mahali popote.
“Kuna umuhimu wa kujifunza na kujua kiundani masuala haya kwakuwa kuna nchi zimefika mbali hivyo na sisi tuwekeze huku. Cloud ni bora kwa upande wangu kwa kuwa inapunguza mawazo katika utumiaji wake,” amesema.
Naye Gabriel Mwongera kutoka kampuni ya Oracle, amesema suluhisho jipya la Oracle lenye uwezo wa kutumia AI ndani ya mifumo yake, hali inayoongeza ufanisi mkubwa katika utunzaji, uchakataji na usimamizi wa taarifa kwa taasisi za kisasa.