Waziri Bashiru Akutana na Wafugaji, Aahidi Mageuzi ya Sekta – Global Publishers



Waziri wa Mifugo na Uvuvi Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amekutana na Sekretarieti ya Chama cha wafugaji nchini ikiwa ni takribani siku mbili tu tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo ambapo amewaelekeza kuhakikisha wanalinda mafanikio yaliyopatikana kupitia sekta ya Mifugo.

Katika kikao hicho kilichofanyika Novemba 20,2025 kwenye Ofisi za Wizara hiyo zilizopo eneo la Mtumba jijini Dodoma, Balozi Dkt. Bashiru amesema kuwa sekta za uzalishaji ikiwemo Mifugo na Uvuvi ndio nguzo ya kulifanya Taifa lijitegemee kiuchumi na kutekeleza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mhe. Dkt. Sami Suluhu Hassan.

“Tunategemea sekta ya Ufugaji itoe mchango mkubwa katika uendeshaji na ukuzaji wa uchumi wetu na kuboresha maisha ya watu wetu” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.

Aidha Balozi Dkt. Bashiru ameelekeza kutoanzishwa kwa miradi mipya Wizarani hapo hadi itakapokamilishwa ile iliyoanzishwa awali na kuanza kufanya kazi iliyokusudiwa.

“Najua ipo miradi imekamilika lakini haijaanza kufanya kazi hivyo tutafanya uchambuzi tuainishe maeneo ambayo tayari fedha za umma zimeshawekezwa na malengo yalikuwepo lakini miradi hiyo haijaanza kuleta matokeo ili tuhakikishe inafanya kazi na ile ambayo haijakamilika tunakamilisha na wakati huo huo tunaanza miradi mipya na hayo ni maelekezo ya Mhe. Rais kwa sekta zote ” Ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji nchini Bw. Murida Mshota amemuahidi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru na Naibu Wake Mhe. Ng’wasi Kamani kuwapa ushirikiano wa kutosha katika kipindi chote watakachohudumu katika nafasi hiyo ambapo pia aliwakabidhi viongozi hao rasimu ya wafugaji inayoelezea mipango mbalimbali ya uboreshaji wa sekta hiyo inayotarajiwa kutekelezwa na wafugaji kote nchini.