Zanzibar. Imeelezwa kuwa, Zanzibar inaendelea kushuhudia mabadiliko ya namna vijana wanavyopata elimu na huduma za afya ya uzazi, hatua inayochangia kupungua kwa vifo vya kinamama na kuongezeka kwa matumizi ya uzazi wa mpango katika jamii.
Mabadiliko hayo yameelezwa kuchochewa na utekelezaji wa Mradi wa Start Small, unaoratibiwa na MSI Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Vijana Zanzibar (Zafyco) na Wizara ya Afya Zanzibar.
Kupitia mradi huo, maelfu ya vijana waliopo katika jamii, shule na vyuo vikuu wamefikiwa na huduma pamoja na elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi.
Mradi huo umejikita katika kuvunja unyanyapaa, kutoa taarifa sahihi na kujenga mazingira rafiki kwa vijana kupata huduma bila hofu.
Jitihada hizo zimeleta mabadiliko makubwa katika mitazamo, tabia na matumizi ya huduma za afya ya uzazi.
Mradi wa Start Small ulianzishwa baada ya tafiti kuonesha ongezeko la mimba zisizotarajiwa, maambukizi ya magonjwa ya zinaa na utoaji mimba usio salama, changamoto zilizokuwa zikiathiri kwa kiasi kikubwa wanafunzi, hususan wa elimu ya juu.
Mkurugenzi wa Zafyco, Abdalla Abeid akizungumza na Gazeti la The Citizen hivi karibuni, amesema awali hali ilikuwa mbaya kuliko ilivyokuwa ikionekana, kwa sababu vijana wengi walikuwa wakikosa taarifa sahihi na kukumbwa na hofu au unyanyapaa wanapotaka kupata ushauri na huduma.
“Hofu, unyanyapaa na taarifa zisizo sahihi ziliwazuia vijana kutafuta huduma. Hata wanafunzi wa sekondari hukabiliana na changamoto hizi,” amesema Abeid.
Amesema mojawapo ya matatizo yaliyobainika ni matumizi mabaya ya vidonge vya P2, huku baadhi ya wanandoa wakiamini kuwa, huduma za uzazi wa mpango zimeandaliwa kwa vijana wasiooana pekee.
Meneja wa Mradi wa Start Small, Domitira Masalla amesema mbinu bunifu kama uhamasishaji wa nyumba kwa nyumba na uanzishaji wa vilabu shuleni, vimekuwa msingi wa mafanikio ya mradi huo.
“Tuliunda maeneo salama ambayo wanafunzi wanaweza kujadili masuala ya afya ya uzazi bila hofu au kuhukumiwa,” amesema.
Masalla amesema mradi haukuishia katika kutoa elimu ya afya ya uzazi pekee, bali pia ulijikita katika mafunzo ya ujasiriamali na stadi za maisha.
Wadau wa sekta ya vijana wamesema hatua hizo zimekuwa muhimu kwa sababu zinawawezesha vijana kupanga maisha yao, kujitambua na kufanya uamuzi sahihi kuhusu afya na mustakabali wao kwa jumla.
Katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), elimu hiyo imeonekana kubadili mtazamo wa wanafunzi wengi.
Naibu Waziri wa Afya na Mazingira, Thani Othman Abdulrahman ambaye pia amefikiwa na shughuli za mradi chuoni hapo, amesema programu hizo zimekuwa nguzo muhimu kwa vijana kujitambua na kujikinga na hatari zinazoweza kuathiri safari yao ya masomo. “Wanafunzi wengi husita kutafuta msaada, wengine huacha masomo kutokana na ukatili au mimba za mapema. Mradi huu unasaidia kupunguza hatari hizo,” amesisitiza Thani.
Katika Wilaya ya Kusini Unguja, huduma za uzazi wa mpango zinaelezwa kupiga hatua baada ya wahudumu wa afya kupatiwa mafunzo maalumu.
Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Mohammed Mtumwa Mnyimbi amesema uzazi wa mpango umekuwa nguzo muhimu katika kupunguza vifo vya kinamama na kuboresha afya ya familia.
Mohammed amesema kiwango cha upatikanaji na matumizi ya huduma kiliongezeka kutoka wastani wa asilimia tisa hadi 12 mradi ulipoanza na sasa kimefikia asilimia 13.9.
Muuguzi na mkunga, Siwangu Steven Muhagama amesema kuongezeka kwa uelewa kumesababisha matumizi zaidi ya njia za uzazi za muda mrefu kama vipandikizi na IUDs.
“Kabla nilihudumia wastani wa watu 16 kwa siku, sasa ni zaidi ya 25,” amesema Siwangu.
Baadhi ya wanufaika akiwamo Christina Ayubu Stefano wa Mwela, amesema huduma hizo zimeleta mabadiliko makubwa katika kupanga maisha.
“Unanipa muda wa kufanikisha mipango yangu kabla ya kupata ujauzito mwingine. Huduma wanazotoa ni za huruma na ushauri mzuri,” amesema Christina.
Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Zanzibar, Saida Abuubakar Mohammed amesema mradi huo umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya kinamama kupitia kuimarisha vituo vya afya, kutoa elimu sahihi na kupambana na imani potofu zinazozuia wanawake na vijana kupata huduma.
Saida amesema vifo vya kinamama vimeshuka kutoka 89 mwaka 2023 hadi 45 mwaka 2025, mafanikio yanayoonesha jinsi elimu na huduma za afya ya uzazi zilizoboreshwa zinavyoweza kuleta mabadiliko ya haraka.
Aidha, kiwango cha matumizi ya uzazi wa mpango kimeongezeka kutoka asilimia 15 hadi 17.5, hatua inayoiweka Zanzibar katika mwelekeo mzuri kuelekea kufikia lengo la kitaifa la asilimia 20 ifikapo mwaka 2030.
Hata hivyo, amebainisha kuwa, bado kuna changamoto, ikiwamo maeneo ambayo hayajafikiwa licha ya uwepo wa vituo 156 vya afya ya mama na mtoto.
“Mwanamke anaweza kuanza uzazi wa mpango hata baada ya kujifungua. Tukitumia ipasavyo, tunaweza kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika,” anasisitiza.
Kadiri Zanzibar inavyosonga mbele kufikia lengo la kutokomeza vifo vya uzazi ifikapo 2030, mradi wa Start Small unaendelea kuwa chachu ya mabadiliko kwa kutoa elimu, kuimarisha huduma na kuwawezesha vijana kupanga mustakabali wao kwa usalama na afya bora.