Bidhaa zaanza kupanda bei kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka Kilimanjaro

Moshi. Wakati msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka ukikaribia, bei za bidhaa mbalimbali za vyakula, ikiwemo mchele, mafuta ya kupikia na maharage, zimeanza kupanda katika masoko ya Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Gazeti Mwananchi limetembelea masoko ya Mbuyuni na Soko Kuu la Moshi, limeshuhudia ongezeko hili la bei, huku baadhi ya wafanyabiashara wakitoa wito kwa wasambazaji wakubwa kuongeza kiwango cha usambazaji wa bidhaa ili kupunguza upungufu unaojitokeza masokoni.

Kawaida, msimu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya huleta idadi kubwa ya wageni mkoani Kilimanjaro, wakiwemo wanaorejea nyumbani kwa mapumziko.

Kuongezeka kwa watu huongeza mahitaji ya bidhaa muhimu, hali inayochangia kupanda kwa bei na wakati mwingine kusababisha uhaba wa bidhaa.

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wafanyabiashara wamesema kuwa mchele umeongezeka bei kutoka Sh3,500 kwa kilo hadi kufikia Sh3,800, huku bidhaa nyingine pia zikionyesha mwenendo wa kupanda bei.

Mmoja wa wafanyabiashara wa Soko Kuu la Moshi, Albina Komu amesema kuwa kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka, bei huenda juu kutokana na mahitaji makubwa ya bidhaa.

“Kwa kipindi hiki ambacho tunakaribia  sikukuu za mwisho wa mwaka,  tumejiandaa vizuri kwa ajili ya biashara, lakini bei za bidhaa sasa hivi ziko juu, mfano mchele ambao ulikuwa unauzwa Sh3,500 sasa hivi unauzwa Sh3,800. Maharage sasa hivi yamepanda hadi Sh4,000 kwa kilo moja kutoka Sh3,000,” amsema mfanyabiashara huyo.

Amesema bidhaa nyingine zilizopanda bei ni mahindi, ambapo sado moja ya mahindi iliyokuwa ikiuzwa Sh3,000 kwa sasa inauzwa Sh3,500.

Venance Mkenda ambaye ni mfanyabiashara wa bidhaa mbalimbali Mjini Moshi, amesema licha ya bidhaa hizo kupanda bei wamejipanga kupokea wateja wengi kuelekea sikukuu hizo za mwisho wa mwaka.

” Tumejipanga vizuri, wateja waje tupo, tunaamini mpaka kufikia sikukuu,  kwenye mafuta na mchele kidogo bei  zipo juu, ila  kwenye mbogamboga na matunda hakuna shida kabisa,”amesema Mkenda.

Kwa upande wake, Katibu wa Soko Kuu la Moshi, George Sizya amesema kuwa hali ya biashara kwa sasa ni tulivu, ingawa changamoto ya kupanda kwa bei imeanza kujitokeza.

Amesema ongezeko hilo la bei linachangiwa na upungufu wa bidhaa sokoni pamoja na kuongezeka kwa mahitaji katika msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.

Sizya amesema mchele, ambao kwa sasa unauzwa kati ya Sh2,500 hadi Sh3,500 kwa kilo kulingana na daraja, unatarajiwa kupanda hadi  Sh3,900 wakati wa sikukuu za mwisho wa mwaka endapo mahitaji yataongezeka bila kuongezeka kwa usambazaji.

Amesema bidhaa nyingine zinazotarajiwa kupanda bei ni pamoja na mafuta ya kupikia, sukari na sabuni, ambapo tayari sabuni zimeanza kupanda bei  sokoni.

“Kwa sasa, mche wa sabuni unauzwa Sh3,500 hadi Sh4,000, huku baadhi zikifikia Sh5,000, ikilinganishwa na bei ya awali ya Sh2,000 hadi 3,000. Vilevile, bei ya katoni ya sabuni imepanda kutoka Sh45,000 hadi Sh76,000,” amesema Sizya.

Sizya ametoa wito kwa wafanyabiashara wakubwa kuingiza bidhaa kwa wakati ili kusaidia kupunguza uhaba unaosababisha kupanda kwa bei.

Amesema pale bidhaa zinapokuwa pungufu, mfumuko wa bei huongezeka, lakini zikiwa zinapatikana kwa wingi, ushindani wa soko huwa mzuri na rafiki kwa watumiaji.