Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametaja baadhi ya huduma zinazotolewa na Serikali ambazo zisipotolewa kwa hakika zinaweza kusababisha wananchi wakaichukia Serikali.
Amesema kukosekana kwa huduma ya maji, rushwa kwa makundi kama bodaboda, suala la mikopo ya asilimia 10 watu kuombwa rushwa, huduma mbovu ikiwemo kujibiwa vibaya na watoa huduma hospitali, mambo haya yanaweza kufanya watu wakachukia Serikali yao.
Ameyasema hayo leo Novemba 24, 2025 eneo la Mbezi kwa Yusuph Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam wakati akizungumza mbele ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, kwenye ziara kwenye vituo vya mwendokasi barabara ya Kimara-Mbezi.
Chalamila ameyasema hayo akirejea vurugu za Oktoba 29, 2025 ambapo ametaja athari zilizojitokeza ikiwemo kuchomwa moto kwa vituo vya mabasi yaendayo haraka maarufu mwendokasi na ofisi za Serikali.
“Ni kweli wananchi yapo mambo ambayo wanayachukia, sisi kama viongozi wa Serikali lazima tusimame kidete katika kushughulikia mambo haya.
“Lazima tuhakikishe Mtanzania huyu haichukii Serikali nikuhakikishie hapa Dar es Salaam lazima tujipange upya na kama wapo Watanzania wanaoichukia Serikali kwa sababu ya mambo haya ya mikopo tutahakikisha faraja inarudi,” ameahidi.
Akieleza zaidi amesema katika siku ya uchaguzi mkuu yalitokea makundi yaliyosababisha athari kama kuchomwa moto kwa vituo vya mwendokasi yaliyosababisha hadi leo mwendokasi imesimama.
Chalamila amesema athari zilizotokea Oktoba 29, 2025 zilitokea kutokana na makundi ya kihalifu ambapo uharibifu umegusa mali za umma na binafsi.
Ametaja kituo cha mabasi cha Magufuli kilikuwa ndiyo kinalengwa kwanza kuchomwa moto, kisha magari ya mwendokasi, vituo vya gesi na jengo la TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania) huku akilishukuru jeshi kuwahi kulinda.
Vituo 20 vya mwendokasi viliharibiwa
Akieleza, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe amesema barabara ya mwendokasi awamu ya kwanza vituo 20 viliharibiwa ikiwemo kuchomwa moto pamoja na kupigwa mawe na kuharibu mfumo ya umeme na mifumo ya kukatia tiketi.
Aonya viongozi wa dini wachochezi
Katika hatua nyingine Chalamila ameonya viongozi wa dini wenye kauli chochezi ambao wamekuwa wakijitokeza katika siku za hivi karibuni.
“Kuna viongozi niliwasikia wanasema suala la kukata watu vichwa mimi naonya na naomba niseme tusifike huku, tuwe viongozi wa dini tunaoelimisha,” amesema.
