Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza kufunguliwa kwa Kanisa la Ufufuo na Uzima, huku akielekeza lipewe miezi sita ya uangalizi kuhusu kuzingatia miiko, masharti na sheria za uendeshwaji wake.
Agizo hilo la Serikali, linakuja ikiwa zikiwa zimepita siku 175 tangu Juni 2, mwaka huu, tangu ilipotangaza kufuta usajili wa kanisa hilo kwa kile ilichoeleza limekiuka masharti ya sheria, kwa madai ya kujihusisha na masuala ya siasa.
Hatua hiyo, ilisababisha waumini wa kanisa hilo kuhama maeneo ya kufanyia ibada ikiwamo barabarani na baadaye kuzuiwa na Jeshi la Polisi.
Askofu wa kanisa hilo, Josephat Gwajima amewahi kueleza kuwa hatua hiyo imevunja haki za waumini, akidai halikupaswa kufungiwa kanisa kwa jumla wake, badala yake anayekosea ndiye afungiwe.
Hata hivyo, agizo la kufunguliwa kwa kanisa hilo, limewaibua waumini wake, waliosema ni taarifa njema na kwamba Mungu ametenda.
Dk Mwigulu ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam leo, Jumatatu Novemba 24, 2025 alipozungumza katika mkutano wa hadhara baada ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na vurugu za Oktoba 29, mwaka huu.
Katika hotuba yake hiyo, amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene pamoja na kanisa hilo, ayaandikie upya makanisa yote masharti na miiko ili yakumbuke taratibu za uendeshwaji wake kwa mujibu wa sheria.
“Natambua lilikuwapo hili moja ya Ufufuo na Uzima kalifungulie. Lifungulie wape masharti ya uangalizi ndani ya miezi sita. Ziandikie taasisi zote za kidini kuzikumbusha miiko na mipaka ya ufanyaji kazi, sawa sawa na sheria na Katiba ya nchi yetu,” amesema Simbachawene.
Sambamba na agizo lake hilo, ametaka masharti yakaangaliwe upya ili akikosea mmoja yasifungwe makanisa yote na kuathiri ibada kwa waumini.
“Ibada ni ushirika kati ya binadamu na Mungu wake, nendeni mkakiangalie vizuri kipengele hicho, ili akikosea sheikh usiadhibiwe msikiti au akikosea askofu wasiadhibiwe waumini wake, wasinyimwe waumini kufanya ushirika na Mungu wao,” amesema.
Simbachawene amesisitiza huo ni msamaha wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa taasisi za kidini zilizokuwa na msukosuko, akitaka ziandikiwe upya miiko na masharti ya uendeshwaji ili zikumbuke mipaka yao.
Mmoja wa wachungaji wa kanisa hilo, Peter Mathias akizungumza na Mwananchi kuhusu kufunguliwa amesema,”habari njema ni kwamba Mungu yupo kazini.
Alipoulizwa kuhusu ibada na wanachoweza kuwaambia waumini wao baada ya kufunguliwa, amesema kama kanisa hawakuwahi kusimama kuacha ibada.
“Sisi ni majasusi wa mbinguni, siku zote mtoto wa simba naye ni simba, kama nilivyosema hatukuwahi kusimama kufanya ibada hata moja, tupo kila muda hata kama haikuwa pale (kanisa la Kibo),” amesema Mathias.
Amesema ibada kwa waumini wa kanisa hilo kipindi chote cha kifungo iliendelea kufanyika kama kawaida, licha ya kutoeleza ni wapi walikuwa wakifanyia.
Awali, walikuwa wakikusanyika barabarani upande wa pili wa kanisa lao na kufanya ibada kabla ya Jeshi la Polisi kuwatawanya na kuhamia kwenye Kanisa la Kiinjili Afrika Mashariki (KKAM) Ubungo Kibo ambako nako walitawanywa na mara kadhaa kupigwa mabomu ya machozi na polisi kabla ya kanisa hilo kuvunjwa.
Mchungaji Mathias ambaye wakati wote alikuwa akitoa salamu ya kanisa hilo la Majeshi Majeshi alipokuwa akizungumza na Mwananchi, amesema wao hawajawahi kupoteza pambano hata moja.
“Aluta continua, majasusi wa mbinguni hatujawahi kupoteza pambano hata moja, tunafahamu usafi unahitajika wa nguvu kanisani, lakini majeshi majeshi yameshinda,” amesema Mathias.
Alipoulizwa kuhusu Askofu mkuu wa kanisa hilo, Josephat Gwajima ambaye kwa muda mrefu hajasikika kuzungumza, amesema yupo salama.
“Baba (Askofu Gwajima) yupo salama kabisa, hana tatizo lolote, bila shaka ibada yake ya kwanza ndani ya kanisa inasubiriwa na wengi na tusishangae ikafunga mtaa, Mungu yupo kazini,” amesema Mathias.
