Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kuendelea na usomwaji wa maelezo ya mashahidi 20 na vielelezo katika kesi ya ubadhirifu na utakatishaji fedha zaidi ya Sh3 bilioni, inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Jatu Public Limited Company (PLC), Peter Gesaya na wenzake saba.
Kesi hiyo imeshindwa kuendelea leo, Jumatatu Novemba 24, 2025 kutokana na hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Geofrey Mhini kuwa na udhuru.
Kutokana na hali hiyo, kesi hiyo imepangwa Novemba 24, 2025 kuendelea na usikilizwaji wa maelezo ya mashahidi na vielelezo( Commital Proceedings).
Kesi hiyo imeahirishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.
Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele alidai kuwa: “Kesi hii imeitwa kwa ajili ya Jamhuri kuendelea na usomwaji wa idadi ya mashahidi na vielelezo, hata hivyo hakimu anayesikiliza kesi hii amepata udhuru, hivyo tunaomba utupangie tarehe nyingine kwa ajili kuendelea na usomwaji wa mashahidi na vielelezo” amedai Mwakamele.
Baada ya kutoa taarifa hiyo, hakimu Lyamuya aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 26, 2025.
Novemba 21, 2025 Jamhuri iliieleza Mahakama hiyo kuwa inatarajia kuwa na mashahidi 60 na vielelezo 136, ambapo mashahidi 40 wameshasomwa maelezo yao na kubaki 20.
Mbali na Gasaya washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 491356 ya mwaka 2023 ni Nicholaus Fuime, Esther Kiya, Habiba Magero, Mariam Mrutu, Mariam Kusaja, Lucy Izengo, na Jatu PLC.
Wote kwa pamoja wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 37, mashtaka matano kati yao yakiwahusu washtakiwa wote na mashtaka 32 yakiwahusu mshtakiwa wa kwanza, Gasaya na wa nane, Jatu PLC peke yao.
Mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao ni kuongoza genge la uhalifu, matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu na kuisababishia hasara mamlaka, huku mengine 33 yakiwa ni ya utakatishaji fedha.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Januari Mosi, 2019 hadi Desemba,2021 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo mengine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika shtaka la kwanza washtakiwa wote wanadaiwa kuwa waliandaa genge la kihalifu kwa nia ya kufanya ubadhilifu wa fedha kiasi cha Sh3,149,172,167 (zaidi ya Sh3.1 bilioni) mali ya Jatu Savings and Credit Cooperative Society Limited.
Katika shtaka la pili, mshitakiwa wa kwanza (Gasaya) na wa pili (Fuime), wanadaiwa kuwa Februari 28, 2019 Dar es salaam katika utekelezaji wa majukumu yao kama Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa Jatu Saccos na Jatu PLC walitumia vibaya nafasi zao kwa kusaini makubaliano (MOU) kati ya Jatu PLC na Jatu Saccos.
Wanadaiwa kusaini mkataba huo kinyume na Kanuni za Vyama vya Ushirika za Mwaka 2015 na Vyama vya Akiba na Mikopo za Mwaka 2019 na kusababisha Jatu PLC kupata faida isiyostahili yenye thamani ya zaidi ya Sh3.1 bilioni.
Shtaka la tatu liliwahusu washitakiwa sita, wa pili hadi wa saba.
Wanadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2019 na Desemba 31, 2021 ndani ya Mkoa wa Dar es salaam wakiwa watia saini wa akaunti ya benki ya NMB ya Jatu Saccos bila uaminifu walitumia kwa masilahi yao binafsi zaidi ya Sh63 milioni mali waliyoaminiwa kwa nafasi zao.
Shtaka la nne, ambalo ni la kusababisha hasara linawahusu washtakiwa wote.
Wanadaiwa kuwa katika tarehe na eneo tajwa hapo juu washtakiwa wote kwa vitendo vyao vya makusudi walisababisha Jatu Saccos kupata hasara ya kifedha kwa kujihusisha moja kwa moja katika miamala ya zaidi ya Sh3.1 bilioni, wakijua kuwa fedha hizo ni matokeo ya kosa la msingi yaani ubadhilifu na matumizi mabaya ya mali.
Shtaka la tano ambalo ni la utakatishaji fedha linawahusu washtakiwa wote.
Wanadaiwa kuwa kwa nyakati tofauti kato ya Januari Mosi, 2019 na Desemba 31, 2021 walijihusisha moja kwa moja katika miamala ya kifedha inayohusisha zaidi ya Sh3.1bilioni, huku wakijua kuwa wakati wanajihusisha na miamala hiyo ilikiwa ni mazao ya kosa tangulizi la ubadhirifu.
Mashtaka 32 ya utakatishaji fedha kuanzia la 6 mpaka la 37 yanamkabili mshtakiwa wa kwanza, Gasaya na wa nane, Jatu PLC wakidaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Julai 1, 2017 hadi Februari 25, 2025.
Wanadaiwa kuwa katika kipindi hicho walinunua mali mbalimbali zikiwemo magari, pikipiki, trekta na shamba.
